Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, akiwa katika wadhifa wake wa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayojishughulisha na Masuala ya Maji Barani Afrika (Global Water Partnership – Southern Africa and Africa Coordination Unit – (GWPSA – Africa)), ameshiriki katika “Siku ya Maji” ya Mkutano wa Sayansi uliofanyika pembezoni mwa Mkutano wa 79 wa Umoja wa Mataifa, jijini New York, Marekani.
Akihutubia washiriki wa mkutano huo, Rais Mstaafu Kikwete aliweka wazi changamoto kubwa zinazokabili sekta ya maji barani Afrika, akibainisha kuwa bara hilo bado linakabiliwa na upungufu mkubwa wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa mamilioni ya watu. Alisisitiza kuwa bila uwekezaji wa haraka na endelevu, lengo la kufikia upatikanaji wa maji kwa wote huenda lisitimie.
Mhe. Kikwete alitoa wito kwa nchi za Afrika na wadau mbalimbali duniani kuendelea kuwekeza katika Mpango wa Maji wa Afrika, akisema kuwa uwekezaji huo ni muhimu kwa kuboresha upatikanaji wa maji safi, salama, na toshelevu barani Afrika. “Maji ni uhai, na bila maji hakuna maendeleo. Afrika inahitaji kushirikiana na wadau wa kimataifa kuhakikisha rasilimali hii muhimu inapatikana kwa wote, hususan katika maeneo ya vijijini ambako changamoto ni kubwa zaidi,” aliongeza.
Pia, Rais Mstaafu Kikwete alionyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na za umma, akisisitiza kuwa suluhisho la changamoto za maji linahitaji ushirikiano wa kimkakati. Alihimiza serikali za Afrika kuwekeza zaidi katika miundombinu ya maji, na kuwataka wadau wa kimataifa kuongeza misaada ya kifedha na kiufundi ili kufanikisha miradi ya maji yenye athari kubwa kwa jamii.
Katika hotuba yake, alibainisha pia umuhimu wa kuhifadhi vyanzo vya maji na kuhimiza matumizi bora ya rasilimali za maji, ili kuhakikisha kuwa vizazi vijavyo navyo vinanufaika na rasilimali hii. “Ni lazima tuwe na mikakati ya muda mrefu itakayohakikisha kuwa tunalinda vyanzo vya maji na kutumia maji kwa njia endelevu,” alisema.
Ushiriki wa Mhe. Kikwete katika mkutano huo unadhihirisha juhudi zake endelevu za kusukuma mbele ajenda ya maji barani Afrika, na dhamira yake ya kuona bara hili linafikia malengo ya maendeleo endelevu katika sekta ya maji.