Na Hamis Dambaya, NCAA
Serikali imewapongeza wananchi wa tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha kwa kuendelea kudumisha umoja, amani na utulivu katika eneo hilo na hivyo kuendeleza falsafa ya R4 ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka wananchi wote kuishi kwa maelewano na maridhiano.
Akizungumza mara baada ya ibada ya shukrani iliyofanyika katika Kanisa katoliki la Mtakatifu Luka lililopo katika kata ya Endulen wilayani Ngorongoro mkoani Arusha mshauri wa Rais wa masuala ya siasa na uhusiano wa jamii balozi Rajab Luhwavi amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amefurahishwa na utulivu mkubwa walioonesha wananchi wa tarafa hiyo na kusema serikali inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yake yote katika eneo hilo
Balozi Luhwavi amewataka wananchi wa Endulen na Ngorongoro kwa ujumla kuendelea kuwa wavumilivu wakati serikali katika ngazi mbalimbali ikiendelea kutekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais huku akisisitiza umuhimu wa wananchi hao kuendelea kupendana na kushirikiana na serikali katika shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ( NCAA) Dkt. Elirehema Doriye amewaambia wananchi hao kuwa Mamlaka yake itasimamia na kutekeleza maelekezo yote yanayoihusu mamlaka hiyo yaliyotolewa na wawakilishi wa mheshimiwa Rais na kwamba hatua mbalimbali zimechukuliwa katika kutekeleza maelekezo hayo ikiwa na pamoja na kuendeleza uhusiano wa NCAA na wananchi wa Ngorongoro.
Kwa upande wake mbunge wa Ngorongoro Mheshimiwa Emmanuel Ole Shangai ameipongeza serikali kwa kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo inatekelezwa na kusema kuwa ataendelea kusimamia suala hilo ili kuleta maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo.
Mheshimiwa Ole Shangai amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kutokana na upendo wake mkubwa kwa wananchi wa Tarafa ya Ngorongoro uliopelekea wananchi wa eneo hilo kuruhusiwa kushiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa baada ya kutolewa tangazo la kufuta vijiji katika tarafa hiyo.
Akizungumza napema katika ibada hiyo Paroko wa kanisa katoliko Endulen Padri Albano Mwombeki amewaongoza wananchi hao katika ibada hiyo ya shukranI na kuwataka kuendelea kudumisha amani,utulivu na mshikamano ili waweze kujiletea maendeleo yao na taifa kwa ujumla.