Na Mwandishi wetu, Babati
WAHITIMU wa darasa la saba wa Tarangire Pre & Primary English Medium School ya mtaa wa Wang’waray mjini Babati wamefanya mahafali ya sita ya kuhitimu darasa la saba kwenye hifadhi ya Taifa ya Tarangire huku wakitalii na kuona wanyamapori wakiwemo tembo.
Katika mahafali hayo ya sita yaliyofanyika ndani ya hifadhi ya Taifa ya Tarangire iliyopo mkoani Manyara, miongoni mwa wahitimu hao 28 walipatiwa zawadi mbalimbali kwa washindi na vyeti kwa wahitimu.
Wahitimu hao 28 wamejumuika na wanafunzi wenzao 18 wanaowakilisha wanafunzi wa madarasa yanayobaki, walimu 15, wafanyakazi wasio walimu 16 wanaojumuisha wahasibu, watunza stoo, madereva, watunza watoto na walinzi.
Mkurugenzi wa shule hiyo CPA, Ronald Paul ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mahafali hayo, amewapongeza wanafunzi waliohotimu kwani muda wote wanajiamini na anatarajia watafaulu vyema katika mitihani yao.
“Nawapongeza wahitimu wa shule hii ya Tarangire ambao kwa muda wa miaka saba mlikuwa mnasoma elimu ya msingi nawatakia kila la heri katika kuendelea na elimu ya sekondari,” amesema CPA Ronald.
Amewapongeza walimu kwa kutimiza wajibu wao ipasavyo kwa ufundishaji na wazazi na walezi kwa kuwalipia ada wanafunzi na kufuatilia masomo yao kupitia uongozi wa shule.
“Walimu wa Shule hii nawapongeza kwa kukunjua mioyo pamoja na miili yao na kuwafundisha wanafunzi hao na kuwafanya kujiamini katika kufanya mitihani mbalimbali,” amesema CPA Ronald.
Amefafanua kuwa mwaka huu mfumo wa mtihani ulikuwa tofauti na miaka iliopita kwani mtihani ulikuwa ni wa kuonesha uelewa wa mwanafunzi na maswali mengi yalikuwa ya kuonesha njia na kutoa jibu au kujieleza tofauti na kuchagua jibu sahihi.
“Wakazi mbalimbali wa Manyara, wazazi na wasimamizi wamekuwa wakiwasifu wanafunzi wa shule hii kwa kutobabaika katika mitihani mbalimbali iliyofanyika shuleni kwetu kutokana na ufundishaji mzuri, wenye weledi na uzoefu wa walimu wetu,” amesema CPA Ronald.
Hata hivyo, baadhi ya wakazi wa mji wa Babati wameielezea shule ya awali na msingi Tarangire kuwa ni shule bora yenye kufundisha taaluma bora, nidhamu na uadilifu kwa wanafunzi wake.
Mmoja kati ya wakazi wa mtaa wa Wang’waray Abdalah Mgeni amesema shule hiyo imekuwa miongoni mwa uwekezaji mzuri uliofanyika kwneye mtaa huo hivyo jamii ichangamkie fursa kwa kuwapeleka watoto wao wakapate elimu.
“Watoto wa shule ya awali na msingi Tarangire wanafundishwa vizuri, wanakula vyakula vizuri na wanalala sehemu nzuri huku mazingira ya shule hiyo yakiwa tulivu na yakupendeza,” amesema.