Na Ashrack Miraji (Fullshangwe Media), Lushoto, Tanga
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Batilda Buriani, ametoa wito kwa wakazi wa mkoa wa huo na Watanzania kwa ujumla kujenga tabia ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, hususan vile vinavyopatikana wilayani Lushoto. Ametaja kuwa kufanya hivyo si tu kunawapatia fursa ya kujifunza kuhusu historia, tamaduni, na mazingira, bali pia huwapa nafasi ya kupumzika, kufurahia uzuri wa asili, na kuchangia kukuza pato la taifa.
RC Batilda alitoa wito huo tarehe 21 Septemba 2024, wakati akikagua maandalizi ya mwisho kuelekea kilele cha “Usambara Tourism Festival” kinachotarajiwa kufanyika wilayani Lushoto Jumapili, tarehe 22 Septemba 2024. Mgeni rasmi katika sherehe hizo anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Dotto Biteko, ambapo hafla itafanyika katika viwanja vya Nyerere Square.
Akiwa katika hifadhi ya msitu wa Magamba na vivutio vya Kiguluhakwewa, Dkt. Batilda alieleza kuwa wilaya ya Lushoto ni moja ya maeneo yenye vivutio bora vya utalii vinavyovutia wageni kutoka mataifa mbalimbali. Kwa mwaka jana, inakadiriwa kuwa takribani watalii 5,000 walitembelea wilaya hiyo.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, amezindua ofisi ya Umoja wa Waongoza Watalii Lushoto. Aliahidi kuwa mlezi wa kituo hicho na kuwataka waongoza watalii kuongeza elimu na kuwa wakarimu kwa wageni wanaowapokea na kuwatembeza katika vivutio hivyo.
Awali, waongoza watalii hao, wakiwasilisha risala yao mbele ya Mkuu wa Wilaya, waliomba kutatuliwa kwa changamoto kadhaa, ikiwemo upatikanaji wa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa utalii.