NA BALTAZAR MASHAKA,MWANZA
KAMATI ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, imelaani vitendo vya mauaji, utekaji, watu kupotea na vitendo vya ukatili vinavyoendelea kutokea na kuripotiwa nchini.
Kamati hiyo iliyokutana leo jijini humo ikiadhimisha Siku ya Amani Duniani huku ikivitaka vyombo vya ulinzi na usalama kutokata tamaa na badala yake viendelee kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo Mchungaji wa Kanisa la EAGT Kiloleli Mwanza, Dk.Jacob Mutashi amewataka vijana kutojiingiza katika mihemko inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani,pia viongozi wa dini wasiwe upande wowote wa itikadi za kisiasa.
“Kamati inalaani vitendo vyote vya mauaji, kupotea kwa watu, kutekwa na ukatili wa aina zote,pia kamati inaiomba serikali kutumia nguvu zake zote katika kukomesha matendo hayo,” amesema Dk. Mutash na kuongeza;
“Tunajitambua kuwa ni wadau wa amani na wabia wa serikali katika maeneo mengi,tuna watu katika nyumba za ibada na jukumu letu ni kushughulikia viashiria vya uvunjifu wa amani kabla ya matatizo kutokea,hivyo Siku ya Amani Duniani hatuwezi kukaa pembeni katika kuhamasisha amani.”
Pia ameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kutokata tamaa badala yake viendelee kufanya kazi zao kwa mujibu wa sheria bila kujali kauli zozote zisizo za msingi.
Kwa mujibu wa kamati hiyo viongozi wa dini katika nyumba zao za ibada watengeneze ratiba ya kuliombea taifahuku wakiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika daftari la wapiga kura linalotarajia kuanza Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu.
Aidha Mchungaji Mutash kwa niaba ya kamati amewahimiza Watanzania kukataa na kukemea vitendo vya rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa na kuhimiza umuhimu wa kuchagua viongozi bora watakaoweza kuleta maendeleo endelevu katika jamii.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Mwanza ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa kamati hiyo, Hasani Kabeke amewataka vijana kuacha kufanya uamuzi kwa kukurupuka na badala yake watafakari kwanza na kuchukua tahadhari juu ya mambo wanayoamua.
Amesema vijana ni hazina kubwa na hakuna taasisi au kada imeimarika bila kundi hilo,ni muhimu wawe watu wenye uamuzi sahihi, wasikurupuke na wawe watu wa akili za kuambiwa changanya na zako na kuchukua tahadhari kwanza kuangalia maisha yao, familia na ya jamii yao pia wawe makini katika kuyaendea mambo.
“Wito wetu kwa Watanzania wote,serikali, vyama vya siasa,viongozi wa dini na waandishi wa habari ni tuhakikishe tunailinda amani ya Tanzania kwa matendo.Ni fursa muhimu wa kila mmoja kuleta mabadiliko chanya katika jamii kuifanya nchi yetu na dunia amani itamalaki,”amesema
Sheikh Kabeke amesema maazimio hayo yanaonesha umuhimu wa umoja na ushirikiano kuhakikisha amani inatawala,tumwombee Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,nchi naa viongozi mbalimbali,Watanzania wote nchi ipate mafanikio,pia tujiombee viongozi wa dini.
Naye mjumbe Kamati ya Amani Wilaya ya Nyamagana, Saada Abbas ametoa wito kwa wazazi kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kutengeneza kizazi bora kijacho