Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Mhe. Dkt. Tulia Ackson, amesema kuwa upo umuhimu wa mataifa mbalimbali duniani kuboresha na kubadilisha mifumo ya kiutawala na ugawaji bora wa rasilimali ili kuwezesha utekelezaji wa Agenda ya 2030 ya Maendeleo endelevu kwa ufanisi zaidi.
Dkt. Tulia ameyasema hayo wakati akichangia kwenye Mkutano Mkuu wa 79 wa Umoja wa Mataifa (UNGA79) uliofanyika New York nchini Marekani leo tarehe 22 Septemba, 2024. Katika mchango wake amesisitiza kuwa juhudi za kusaidia nchi zinazoendelea kukuza uchumi zinapaswa kuongozwa na mikakati ya kimkakati, hususan katika kugawanya upya rasilimali za kiuchumi.
Dkt. Tulia amebainisha kuwa rasilimali nyingi ziko mikononi mwa wachache kitaifa na kimataifa jambo linalochangia kutokuwepo kwa usawa wa kiuchumi. Hivyo, amehimiza kuwa ipo haja ya kuweka mkazo mkubwa zaidi katika kuhakikisha ugawaji bora wa rasilimali hizo ili kufikia maendeleo endelevu na kupunguza pengo la kiuchumi kati ya mataifa na ndani ya mataifa husika.
Katika hotuba yake, ameonesha bayana kuwa hatua za pamoja zinahitajika ili kuleta usawa wa kiuchumi na kijamii duniani na kuzipa nguvu Serikali za nchi zinazoendelea kufikia malengo ya kiuchumi na maendeleo kwa raia wao.