…………………
Happy Lazaro ,Arusha .
Arusha .Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Wilson Mahera, amekemea vikali tabia ya wazazi wenye tabia ya kuwaficha watoto wenye mahitaji maalumu na kuwanyima haki zao za msingi kuacha tabia hiyo mara moja kwani watoto wote wana haki kama wengine .
Ameyasema hayo mkoani Arusha wakati akimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Miaka ya 30 ya Elimu Jumuishi hapa nchini yaliyofanyika katika chuo cha elimu maalumu Patandi .
Amesema kuwa, watoto wenye mahitaji maalumu wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali zinazosababishwa na wazazi ama walezi wenyewe ikiwemo ya kunyanyapaliwa na kunyimwa haki zao za msingi.
“Nawaombeni wazazi mshirikiane pamoja na serikali kuwaripoti watoto wote wenye mahitaji maalumu waliopo kwenye maeneo yenu ili waweze kupata haki zao za msingi kwenye vituo maalumu ambavyo vimeainishwa na serikali kwani wana haki kama walivyo watoto wengine.”amesema Dkt.Mahera.
Dkt. Mahera amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali ikiwemo utekelezaji wa lengo naomba 4 la malengo ya milenia ya mwaka 2030 linalosisitiza usawa pamoja na kutekeleza Azimio la Musoma la mwaka 1974, ambalo lililochagiza kila Mtanzania kupata fursa ya elimu.
“Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi Serikali imefanikiwa kuyafikia makundi yote ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wanafunzi wenye ulemevu, magonjwa ya kudumu pamoja na wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini.”amesema Dkt .Mahera.
“Tunaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuandaa miongozo inayoelekeza wadau wa elimu kutoa huduma kwa wanafunzi wenye mahitaji Maalumu hususani wenye kiwango kikubwa cha ulemavu” amesema Dkt. Mahera.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anaye shughulikia elimu Atupele Mwambene amewaasa Maafisa Elimu Maalum wa Wilaya kuhakikisha wanaelewa vyema mikakati na miongozo ya utekelezaji wa elimu Jumuishi ili kuwa na ufanisi mzuri wa majukumu yao.
Mwambene amesema Serikali itaitekeleza kwa vitendo na kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu wanajengewa maadili mazuri kwa kuimarisha vituo vya malezi, ushauri na unasihi ili viweze kutoa huduma nzuri.
“Tutaendelea kusimamia utekelezaji wa zoezi la ubainishaji wa Watoto wenye mahitaji maalumu na kuhakikisha wanaandikishwa shule na kupatiwa afua stahiki kulingana na mahitaji waliyonayo”. amesema Mwambene.