Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Timu za Ofisi ya Bunge, Wizara ya Ujenzi na Wizara ya Afya zimeendelea kung’aa kwenye michezo ya mpira wa netiboli, kuvutana kwa kamba na mpira wa miguu katika michuano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara, Wakala na Wakuu wa Mikoa (SHIMIWI), inayoendelea kwenye viwanja mbalimbali mkoani Morogoro.
Timu ya Ofisi ya Bunge imeweka rekodi kwa kufunga magoli mengi zaidi ya timu nyingine zinazoshiriki kwenye michezo hii, ambapo wamefunga Bodi ya Pamba kwa magoli 75-1; wakati timu ya wanaume ya Wizara ya Ujenzi wamewavuta Wizara ya Kilimo kwa mivuto 2-0 na timu ya Wizara ya Afya imewafunga bila huruma RAS Kilimanjaro kwa magoli 8-0 michezo yote imefanyika kwenye uwanja wa Jamhuri.
Katika michezo mingine ya mpira wa netiboli iliyochezwa leo tarehe 22 Septemba, 2024 asubuhi timu ya TAKUKURU wamewafunga Mamlaka ya Usalama na Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) kwa magoli 25-16; nao Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wamewafunga ndugu zao Tume ya Utumishi kwa magoli 47-7; Ofisi ya Ukaguzi wamewaliza Wizara ya Maliasili na Utalii 35-26; Wizara ya Nishati waliwafunga Wizara ya Uchukuzi kwa magoli 32-30.
Katika mchezo wa soka timu ya Wizara ya Mambo ya Ndani wamewafunga Ofisi ya Bunge kwa bao 1-0; timu ya Ofisi ya Rais Ikulu wamewachapa OSHA kwa magoli 2-0.
Katika mchezo wa kuvutana kwa kamba kwa upande wa wanaume timu ya Wizara ya Elimu wamewavuta RAS Lindi (2-0); Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamewavuta Wizara ya Ardhi (2-0); Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wamewavuta RAS Iringa (2-0);Wizara ya Viwanda na Biashara wamewashinda Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji (2-0); Ofisi ya Waziri Mkuu Sera wametoka sare na Wizara ya Maji (1-1) na Ofisi ya Bunge wamepata ushindi wa chee baada ya RAS Simiyu hawakutokea uwanjani.
Michezo mechi nyingine za kamba wanaume timu ya Wizara ya Madini wamewavuta RAS Singida (2-0); nayo Ofisi ya Rais Ikulu wamewavuta timu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa 2-0; Wizara ya Maliasili na Utalii wamepata ushindi wa mezani baada ya Katiba na Sheria kutoonekana uwanjani; timu ya Ofisi ya Maadili ya Viongozi wamewavuta Wizara ya Afya (2-0); nao Mahakama wamewavuta RAS Shinyanga (2-0); timu ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora wamewavuta Wakili Mkuu (1-0); Hazina wamewavuta Tume ya Sheria (2-0).
Michezo ya Wanawake Wizara ya Mambo ya Ndani wametoka sare na RAS Geita (1-1); Wizara ya Maliasili na Utalii wamewashinda Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji (2-0); Wizara ya Mambo ya Nje wamewavuta Wizara ya Kilimo (2-0); RAS Shinyanga wamevutwa na Hazina (0-2); Wizara ya Viwanda na Biashara wamewavuta RAS Singida (2-0); Ofisi ya Waziri Mkuu Sera wamewashinda Tume ya Sheria (1-0); na Ofisi ya Wakili Mkuu wamevutwa na Ofisi ya Mashtaka ya Taifa (0-2).
Michezo mingine ya wanawake Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamewavuta RAS Kilimanjaro (1-0); Wizara ya Katiba na Sheria wamewavuta Haki (2-0); Mahakama wamewavuta UCSAF (2-0); Wizara ya Ardhi imevutwa na Wizara ya Uchukuzi (0-2); Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi wamewavuta Tume ya Utumishi wa Umma (1-0); TAMISEMI wamepata ushindi wa chee baada Bodi ya Bahati Nasibu kutoonekana;nayo RAS Tanga wamewavuta Wizara ya Ujenzi (2-0); Wizara ya Afya wamewavutya RAS Simiyu (2-0).
Michezo hiyo inaendelea kesho tarehe 23 Septemba, 2024 kwenye viwanja vya Jamhuri, Chuo cha Ujenzi, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) Kampasi Kuu na Mazimbu.