* Asisitiza Amani, Uvumilive na Kuheshimiana Miongoni mwa Watanzania
* Serikali Yaipongeza JMAT kwa Kuhimiza Amani Nchini
* Ahimiza Uchaguzi Kuunganisha Watanzania
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amewataka Watanzania kulinda na kudumisha amani iliyopo nchini kwa kuzingatia misingi ya upendo, uvumilivu na kuheshimiana.
Dkt. Biteko ameyasema hayo leo Septemba 21, 2024 jijini Dar es salaam wakati akimwakilisha Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdory Mpango katika Kongamano la Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) katika Siku ya Amani Duniani inayolenga kuifanya dunia kuwa sehemu sala ya kuishi kwa kuhimiza kutunza thamani ya amani na kuzuia migogoro.
Aidha, amewaasa Watanzania kudumisha amani iliyopo nchini ili kutoa fursa kwa nchi na Watanzania kujiendelea kujiletea maendeleo.
Dkt. Biteko amesema kuwa licha ya Mwenyezi Mungu kuibariki nchi ya Tanzania kwa kuwa na eneo kubwa lenye rasilimali pamoja na watu wenye tofauti za imani, kipato na makabila bado ni lazima Watanzania kuendelea kuwa wamoja na kutunza amani kwa kuwa ni msingi wa maisha.
‘’Mungu ametuumba akatuweka katika nchi nzuri na kubwa yenye mita za mraba zaidi ya 900,000, akatupa milima, mabonde na tambarare, Mungu ametupa matabaka ya wenye navyo na wasio navyo, tofauti za umri, makabila, akatuunganisha nchi mbili Zanzibar na Tanzania Bara kuwa nchi moja haya yote yamewezekana na tofauti hizi hazijatupa haja ya kuondoa amani yetu. Tofauti tulizo nazo ni nyingi lakini zisiwe sababu za kutofautiana na kuondoa amani yetu.’’ Amesisitiza Dkt. Biteko.
Ameongeza kuwa ikiwa dini moja au kabila moja likajiona bora kuliko linguine hali hiyo itasababisha uvunjifu wa amani, na kuwa Watanzania wanahitaji kustahimiliana ili kujenga amani ya pamoja.
‘’ Amani ikitoweka wanaoumia si tu wanaosababisha itoweke bali hata wewe unayedhani haikuhusu mataifa yenye migogoro wanatumia fedha za wananchi kwenda kutafuta amani kwa kujadiliana katika nchi zingine, hivyo tuilinde nchi yetu.’’ Amebainisha Dkt. Biteko.
Fauka ya hayo, Dkt Biteko ameitaka JMAT kuwa sehemu ya kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kwa kuhimiza wananchi kugombea na kuchagua viongozi wenye sifa. Aidha, amesema kuwa uchaguzi huo uwaunganishe Watanzania kwa kufanya kampeni za kistaarabu na wagombea kuelezea tofauti zao za mawazo kistaarabu.
Naye, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amoni Mpanjo amesema kuwa amani ni nguzo kuu ya kila jambo na ndio maana Wizara inahimiza amani ndani ya jamii. Aidha, ameipongeza JMAT kwa kuunganisha dini na watanzania na kusema Jumuiya hiyo ni mbia kwa Wizara yake na inasaidia kuwafikia Watanzania, Sambamba na kuasa jamii kuacha vitendo vya ukatili ikiwemo utekaji na ubakaji.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum amesema kuwa lengo la Kongamano hilo la JMAT ni kuiombea nchi ili wanaofanya vitendo vya kihalifu kuacha na wananchi waishi kwa amani na bila hofu.
‘’ Sisi viongozi wa dini tunaamini kupitia maombi amani itaendelea na vitendo viovu vitaisha mafundisho ya dini zetu yote yanatufundisha kuhusu amani,’’ amesema Sheikh Alhad.
Mkurugenzi Idara Kuu ya Fedha, Uchumi na Utekelezaji wa JMAT, Bw. Ayub Sanga amesema kuwa Jumuiya hiyo inashughulika kwa ajili ya amani na maridhiano na inahusisha dini zote ikiwemo Budha na Hindu na kuwa viongozi wake wanatoka katika dini mbalimbali pamoja na viongozi wa mila na desturi ili kupangana vizuri kwa ajili ya kuendelea kudumisha amani nchini.