Na. Anangisye Mwateba-Arusha
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) amezitaka Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kujizatiti katika kuboresha miundombinu ya barabara ili ziweze kupitika wakati wote.
Mhe. Kitandula ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miundombinu ya barabara katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro.
Naibu Waziri alisema sekta ya utalii inaumuhimu mkubwa katika uchumi wa taifa letu kupitia mchango wake kwenye pato la Taifa, na ajira nchini. Ndio maana Mhe. Rais amekuwa mstari wa mbele kuongoza jitihada kubwa za kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania, jitihada ambazo zimezaa matunda kwa kuwepo muitikio mkubwa wa watalii kuja kutembelea nchi yetu. Hivyo kama taifa hatunabudi kuhakikisha huduma zetu zinaboreshwa na kuwa zakiwango cha juu; sambamba na uboreshaji wa barabara na viwanja vya ndege ndani ya hidadhi.
Aidha, katika hatua nyingine alitoa msisitizo kuwa katika mkakati wa muda mfupi lazima TANAPA NCAA kuongeza juhudi za matengenezo ya mara kwa mara ili barabara ziweze kupitika vizuri wakati wote, na pia kuhakikisha usalama kwa wanaotumia barabara hizo na hivyo kuwapunguzia watoa uhuduma gharama za matengenezo ya magari.
Vilevile Mhe. Kitandula alisisitiza kuwa kwa mpango wa muda mrefu wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha tabaka ngumu kutoka geti la Loduare kuelekea Golini, NCAA ihakikishe inakamilisha taratibu haraka ili ujenzi uanze mara moja. Sambamba na barabara hiyo aliwataka TANAPA nao kuharakisha taratibu za kihandisi ili kuwezesha ujenzi wa barabara ya kudumu kutoka Golini – Naabi- Seronera- hadi lango la Ikoma ili iweze kujengwa kulingana na matakwa ya UNESCO.
Katika ziara hiyo ya ukaguzi wa miundombinu ya utalii iliyopo Hifadhi ya Serengeti na mamlaka ya hifadhi ya eneo la Ngorongoro, Mhe. Kitandula ame sisitiza kuwa huduma zinazotolewa lazima ziendane na viwango vya kimataifa. Pia, alisisitiza umuhimu wa kuzingatia uhifadhi wa mazingira wakati wa kuboresha miundombinu ili kulinda urithi wa asili wa hifadhi zetu.
Mhe. Kitandula aliwakumbusha wahifadhi kuhusu umuhimu wa kufuata kanuni, taratibu, na sheria za nchi katika utendaji wa kazi zao. Alisisitiza kwamba kufuata taratibu na sheria hizi si jambo la hiari.