Jeshi la Polisi nchini limeungana na wadau wengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai leo tarehe 20 Septemba 2024, katika Chuo cha Taaluma ya Polisi, Kurasini, Dar es Salaam.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Polisi wa Uchunguzi wa Kisayansi, mgeni rasmi katika hafla hiyo, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Mwamini Rwantale, ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Sayansi Asilia katika Jeshi la Polisi, alisema kuwa hii ni mara ya kwanza kwa Jeshi la Polisi kuadhimisha siku hii muhimu.
DCP Rwantale alisema, “Uchunguzi wa Sayansi ya Jinai umesaidia kuhakikisha haki inatendeka kwa kuwa umesaidia kubaini wahalifu kirahisi na kuwaunganisha na tuhuma zinazowakabili bila shaka, huku wasio na hatia wakiachiliwa huru.”
Aidha, DCP Rwantale aliongeza kuwa maadhimisho haya yanaleta jamii pamoja, kwani uchunguzi wa kisayansi unasaidia katika kutenda haki kwa usahihi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam, DCP Dkt. Lazaro Mambosasa, alisema kuwa uchunguzi wa kisayansi unahakikisha hakuna mtu anayeadhibiwa bila hatia, na hivyo unaleta taswira njema kwa Jeshi la Polisi na Serikali katika kutenda haki.
Naye Afisa kutoka Mamlaka ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Bw. Fidelis Sekumba, alisema kuwa uchunguzi wa kisayansi unatoa ushahidi wa uhakika zaidi na kurahisisha maamuzi ya kisheria katika mihimili inayohusika kutoa haki.
Maadhimisho haya hufanyika kila mwaka tarehe 20 Septemba, yakiwaunganisha wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi katika juhudi za kutanzua uhalifu.