Na WAF – Ruvuma, Songea
Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songea itawezesha upatikanaji wa huduma za ubingwa bobezi ikiwemo huduma za magonjwa ya akina mama na uzazi, magonjwa ya Upasuaji, magonjwa ya Ndani, magonjwa ya Watoto, magoniwa ya Kinywa na Meno, Macho, Masikio, Pua na Koo pamoja na huduma ya Mionzi.
Waziri Mhagama amesema hayo leo Septemba 21, 2024 alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo iliyopo katika Kata ya Mwengemshindo, Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ambapo ameambatana na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala na Rasilimali watu, Hospitali za Rufaa za Mikoa Bw. Danny Temba, Mkurugenzi wa huduma za Tiba Dkt. Hamadi Nyembea, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera na Mipango Bw. Tumainieli Macha.
“Awali ili mtu apate matibabu haya ilikua lazima aende Muhimbili, na wakati mwengine ilikua lazima aende kutibiwa nje ya nchi, uwezo wetu kwa wananchi wengi ni mdogo, Serikali itakusaidia kumtibu mgonjwa lakini kumuuguza ni garama nyingine, huduma hizo kwa sasa zinapatikana hapa hapa Mwengemshindo ili kuokoa garama za mwananchi kutafuta tiba.” Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amesema jengo hilo limekaa muda mrefu bila kukamilika, hivyo amekabidhi hundi ya fedha kiasi cha Shilingi Milioni 283,467,765.60/= ili apewe mkandarasi aendelee na ujenzi wa Hospitali hiyo ambayo ameelekeza ikamilike katika maeneo ambayo bado hayajakamilika kabla ya mwezi Februari 2025 huduma zianze kutolewa.
Aidha, Waziri Mhagama amesema ndani ya miaka Mitatu ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanyika uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Afya ikiwemo miundombinu ya majengo ambapo ametoa Shilingi Bilioni 3.8 ili kujenga Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Songea, ununuzi wa vifaa, vifaa tiba ikiwemo mashine za MRI pamoja na CT-Scan. I
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwekeza mradi wa ujenzi wa Hospitali hii ya Rufaa ili kiu ya wananchi wa Kata ya Mwengemshindo, wananchi wa Songea na wanaruvuma kwa ujumla ili kuhakikisha wanafikiwa na huduma za Afya zenye viwango.” Amesema Waziri Mhagama
Amesema, Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kutoa huduma za tiba kwa magonjwa hayo ikiwemo magonjwa yanayohitaji huduma za kibingwa zipatikane kwa bei nafuu na inayowezekana kwa kila mwananchi wa Mwengemshindo na Watanzania kwa ujumla.
Waziri Mhagama amewataka wananchi wa Halmashauri ya Manispaa ya Songea kuchagua wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii watakaosaidia kuibua wagonjwa kwenye maeneo yao ambao katika kila mtaa kutakua na wahudumu Wawili (Wakike na Wakiume).
“Wahudumu hawa wa Afya ngazi ya jamii, watapita katika maeneo yetu kutupima, na kama utagundulika kuwa una tatizo lolote la kiafya watakushauri uende hospitali kwa matibabu zaidi, na huduma hizi zitatolewa bila malipo, zitalipiwa na Serikali.” Amesema Waziri Mhagama.