Na Neema Mtuka, Rukwa
Wachimbaji wadogo wa madini katika mkoa wa Rukwa wametakiwa kuchangamkia fursa zilizowekwa na Serikali kwa kuchimba madini kwa njia salama, kulipa kodi kwa wakati, na kuwekeza katika migodi ili kukuza sekta ya madini nchini.
Hayo yameelezwa leo, Septemba 20, 2024, na Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Joseph Kumburu, wakati wa mafunzo na mkutano mkuu wa Chama cha Wachimbaji wa Madini wa Mkoa wa Rukwa (RUREMA). Mafunzo hayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya madini wanaofanya kazi za utafiti, uchimbaji, na biashara ya madini kutoka wilaya za Sumbawanga, Kalambo, na Nkasi.
Mhandisi Kumburu alibainisha kuwa ofisi yake imefanikiwa kutoa leseni zipatazo 245, ikijumuisha leseni 26 za utafiti wa madini, leseni 216 za uchimbaji mdogo, leseni 2 za uchimbaji wa kati, na leseni 1 ya biashara kubwa ya madini.
Pia, alieleza kuwa ofisi yake imekusanya kiasi cha shilingi milioni 499.4 kwa mwaka wa fedha 2023/2024, ongezeko la asilimia 21 ikilinganishwa na kiasi cha shilingi milioni 395.01 zilizokusanywa mwaka wa fedha 2022/2023.
“Ofisi yangu inafanya jitihada kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata maeneo ya kufanya kazi za uchimbaji wa madini kwa urahisi na ufanisi,” alisema Mhandisi Kumburu.
Awali, akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, alikipongeza Chama cha Wachimbaji wa Madini kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu. Alisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuwasaidia wachimbaji wadogo ili waweze kukua na hatimaye kufikia hadhi ya kuwa wachimbaji wa kati na wakubwa.
“Nitoe wito kwa wamiliki wa leseni za utafiti wa madini katika mkoa wa Rukwa, hasa wale waliopokea hati za makosa, kuhakikisha wanaendeleza leseni zao, vinginevyo tutalazimika kuishauri Serikali kuzifuta,” alisema Makongoro.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa RUREMA, Marie Mwambene, alisema ofisi ya madini imeanzisha miongozo mipya ya usimamizi wa madini, ikiwemo kuhakikisha madini yote yanayosafirishwa yanapitia mchakato sahihi wa kupata vibali.
Baadhi ya wachimbaji wadogo waliohudhuria mafunzo hayo, kama Lusia Isaac, walitoa shukrani kwa elimu waliyopata na kuomba mafunzo kama hayo yaendelezwe ili kuongeza uelewa katika sekta hiyo.
“Tunashukuru kwa elimu tuliyoipata leo na tunatarajia kuwa huu utakuwa mwanzo mzuri wa mafunzo mengine zaidi,” alisema Lusia.
Naye Rais wa Shirikisho la Wachimbaji wa Madini Tanzania, John Wambura, aliwataka wachimbaji hao kushiriki katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika tarehe 10 Oktoba 2024 jijini Tanga, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba. Pia aliwasihi wachimbaji kushirikiana na Serikali kwa kulipa kodi na kupanua wigo wa fursa za uwekezaji katika sekta ya madini.
Madini yanayopatikana katika mkoa wa Rukwa ni pamoja na emarald, ruby, zircon, amethyst, makaa ya mawe, chokaa (limestone), mica, aquamarine, appetite, copper, na titanium.