Na WAF – Ruvuma, Songea
Waziri wa Afya na Mbunge wa Jimbo la Peramiho mkoani Ruvuma Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari juu ya magonjwa ya mlipuko pamoja na magonjwa Yasiyoambukiza.
Waziri Mhagama amesema hayo Septemba 20, 2024 alipokua akiongea na watumishi wa Hospitali ya St. Joseph’s mission ambayo ni Hospitali ya Rufaa ya Peramiho alipofanya ziara Hospitalini hapo kwa lengo la kujione hali ya utolewaji wa huduma za Afya.
“Tuendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na magonjwa ya mlipuko kama Mpox, lakini pia kuna magonjwa Yasiyoambukiza kama shinikizo la juu la damu (High Blood Pressure), Kisukari pamoja na magonjwa ya Figo.” Amesema Waziri Mhagama
Aidha, Waziri Mjagama amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uwekezaji mkubwa kwenye Sekta mbalimbali ikiwemo Sekta ya Afya kwa kuwalipa mishahara watumishi, kununua vifaa, vifaa tiba, kuendelea kujenga wodi za watoto wanaozaliwa na uzito pungufu (NCU).” Amesema Waziri Mhagama
“Kwa dhamana hii aliyonipa Mheshimiwa Rais ya kuitumikia Sekta ya Afya, namuahidi nitaendelea kuitumikia kwa moyo wangu wote, na hii ni heshima yetu kwenye jimbo letu la Peramiho kwa ujumla wake.” Ameahidi Waziri Mhagama
Amesema, kwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 3.2 ili kuwaunga mkono Hospitali ya St. Joseph’s Mission ambayo imepewa hadhi kuwa Hospitali ya Rufaa kwa kuwa na madaktari bingwa na bobezi.
“Tutaendelea kuzungumza na wadau wengine ili waendelee kuwekeza kwenye Hositali yetu ya Peramiho, tunaishukuru Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation kwa kulipia watumishi Wanne mishahara, huu ni ushirikiano mzuri na wenye tija.” Amesema Waziri Mhagama
Waziri Mhagama amesema, eneo jingine ambalo Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amelifanyia kazi kubwa ni kuokoa vifo vya kina mama na watoto pindi wanapojifungua ambapo awali takwimu zinaonesha kuwa kati ya wakinamama 1,000 wanaojifungua, 555 walikua wanaooteza maisha.
“Lakini sasa hivi tumepunguza hiyo namba mpaka imefika 104 kwa akina mama 1,000, hiyo ni kazi kubwa ambayo ameifanya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwetu sisi sote kwa pamoja wanawane na wanaume lazima tusimame pamoja tumuunge mkono kwa juhudi hizi anazozifanya kwa Watanzania.” Amesema Waziri Mhagama
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe. Wilman kapenjama Ndile amesema watoto wanaozaliwa na uzito pungufu wanapata huduma bora na nzuri katika Hospitali ya Rufaa ya Peramiho, hospitali hii imeonesha namna ambavyo wanaweza kutoa huduma kwa watoto hao wagonjwa ambao wanahitaji uangalizi wa hali ya juu.”