Balozi wa Tanzania nchini Comoro, Mhe. Saidi Yakubu amefanya mazungumzo na Waziri wa Elimu ya Juu wa Comoro, Mheshimiwa Bacar Mvoulana juu ya kuongeza ushirikiano katika Sekta ya Elimu.
Balozi Yakubu alimueleza Waziri Mvoulana kuwa Tanzania na Comoro tayari zina ushirikiano wa muda mrefu katika Sekta ya Elimu ambapo mwaka 2008 Chuo Kikuu cha Comoro na Chuo Kikuu cha Dar es salaam viliingia makubaliano ya ushirikiano na mwaka 2015 Serikali ya Comoro ilisaini makubaliano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika maeneo kadhaa ya Elumu ikiwemo kubadilishana wataalamu wa lugha za kifaransa, kiswahili na wa vyuo vya ufundi.
Aidha, Balozi Yakubu aliongeza kuwa mwaka jana 2023 Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar kupitia makubaliano yake na Chuo Kikuu cha Comoro kilileta wataalam wa Kiingereza kwa muda wa mwezi mmoja na kumuomba aridhie ili sasa Taasisi za Elimu ya Masafa za Chuo Kikuu Huria na Chuo cha Uhasibu Arusha kuingia makubaliano ya kutoa shahada za uzamili na uzamivu na mafunzo ya kozi za kitaaluma za uhasibu na TEHAMa.
Kwa upande wake, Waziri Mvoulana aliishukuru Tanzania kwa ushirikiano uliopo na kueleza kuwa hivi karibuni watawaalika watalaamu wa Elimu tola Tanzania ili kuendeleza majadiliano na kuwa Comoro iko tayari kwa ushirikiano uliopendekezwa na Balozi Yakubu.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo na maafisa wengine waandamizi.