**†*********
Na Sixmund Begashe -Kilwa
Jitihahada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuifungua zaidi Mikoa ya Kusini kiutalii inashika kasi hususani katika Utalii wa Kihistoria na Malikale kwa kuyapa Mapango ya Nandete na Namaingo hadhi ya kuwa Urithi wa Taifa .
Hili limejidhihirisha kwa namna Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, inavyoshirikiana na Wilaya ya Kilwa na Wakazi wa Nandete kuchechemua Utalii wa Kihistoria na Malikale kupitia Tamasha la miaka 119 la kumbukizi ya Vita ya Maji Maji Katika Kijiji cha Nandete Kilwa.
Akifunga rasmi Tamasha hilo kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi amesema Wizara hiyo itaendelea kuhakikisha kuwa Historia ya Vita ya Majimaji inaendelezwa kuwa miongoni mwa mazao ya utalii ambayo ni nyenzo muhimu ya ajira, kuimarisha umoja, uzalendo na mshikamano miongoni mwa jamii za mkoa wa Lindi, mikoa ya Kusini na Tanzania
nzima.
Dkt. Abbasi amewataka wananchi hususani vijana kuendelea kuwaenzi Mashujaa na Waasisi wa uzalendo kwa Taifa letu na kutekeleza kwa vitendo dhana ya uzalendo kwa kufanya kazi kwa bidii ,kulinda rasilimali za Taifa, kupambana na kuzuia rushwa, ujangili wa wanyama pori na rasilimali nyingine kwa maslahi mapana ya Taifa.
Katika maadhimisho hayo yaliyohudhutiwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohammed Nyundo, Mbunge wa Kilwa Kaskazini Mhe. Francis Ndulane, Mkurugenzi wa Idara ya Malikale Dkt. Christowaja Ntandu, viongozi wa kimila, familia za wapigania uhuru hao na mamia ya wananchi, kwa niaba ya Wizara, Dkt. Abbasi ameahidi watamwomba Rais Samia kusaidia ujenzi wa Makumbusho Maalum ya vita hiyo katika mahali ipoanzia pale Julai 15, 1905, kwa wananchi kung’oa pamba katika shamba la wakoloni wa Kijerumani.
Naye Chifu wa Kabila la Wamatumbi Bw. Omary Shukurrumungu Mbonde ameishukuru Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuyatambua na kuyapa hadhi ya kuwa Urithi wa Taifa Mapango ya Nandete na Namaingo jambo ambalo litahamasisha zaidi Uhifadhi, Ulinzi na kuyatumia zaidi kuvutia watalii.
Katika maadhimisho hayo wadau mbalimbali wamechangia vitu mbalimbali katika maandalizi ya Tamasha kubwa zaidi la mwakani ambapo Vita ya Maji Maji itafikisha miaka 120 ambapo mchele zaidi ya kilo 1,500 umeahidiwa, mafuta zaidi ya ndoo 10, ng’ombe zaidi ya wanne, mbuzi kuku na fedha taslimu.