……………….
Na Mwandishi Wetu, Nandete
Rais wa Awamu ya Sita Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aneelezwa kuwa mmajimui wa Kiafrika anayeenzi mchango wa wapigania uhuru kivitendo ikiwemo historia ya vita ya Maji Maji iliyoazishwa na wazalendo wa kabila la Wamatumbi na kuenea eneo kubwa la jamii za Kusini kupinga ukoloni wa Kijerumani kati ya mwaka 1905 hadi 1907.
Hayo yamesemwa leo kijijini Nandete Kata ya Kipatimu, Kilwa, wakati Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi akifunga Tamasha la kuadhimisha miaka 119 ya Vita ya Majimaji.
“Wazee wetu walioongoza vita ile chini ya Jemedari Mkuu Mzee Kikwako Mbonde na mwanafalsafa wake mkuu na mhamasishaji Mohammed Ali Kinjekitile Ngwale walipandikiza mbegu ya ari ya uhuru na uzalendo ambayo leo Rais wetu Dkt. Samia Suluhu anaienzi kwa kuleta maendeleo,” alisema pia Dkt. Abbasi akiongeza:
“Rais Samia pia anawaenzi wapigania uhuru hawa wa Maji Maji kivitendo kwani ni mwaka huu; miaka 119 baadaye ambapo Serikali yake imeyatangaza rasmi kupitia GN 163 na 166 maeneo ya Nandete yaliyohusika na vita hiyo kuwa urithi wa Taifa na Kimataifa.”
Katika maadhimisho hayo yaliyohudhutiwa pia na Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mhe. Mohammed Nyundo, Mbunge wa Kilwa Kaskazini Mhe. Francis Ndulane, viongozi wa kimila, familia za wapigania uhuru hao na mamia ya wananchi, kwa niaba ya Wizara, Dkt. Abbasi ameahidi watamwomba Rais Samia kusaidia ujenzi wa Makumbusho Maalum ya vita hiyo katika mahali ipoanzia pale Julai 15, 1905, kwa wananchi kung’oa pamba katika shamba la wakoloni wa Kijerumani.
Katika maadhimisho hayo wadau mbalimbali wamechangia vitu mbalimbali katika maandalizi ya Tamasha kubwa zaidi la mwakani ambapo Vita ya Maji Maji itafikisha miaka 120 ambapo mchele zaidi ya kilo 1,500 umeahidiwa, mafuta zaidi ya ndoo 10, ng’ombe zaidi ya wanne, mbuzi kuku na fedha taslimu.