Na Prisca Libaga Maelezo, Mwanga
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Kanda ya Kaskazini kwa kushirikiana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ya Wilaya ya Mwanga tarehe 19.09.2024 imetoa elimu kinga kwa makundi mbalimbali juu ya madhara ya tatizo la dawa za kulevya wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Jumla ya watu 2,500 walipatiwa elimu kinga ikihusisha wanafunzi wa Shule za Sekondari za Mwanga, Vudoi na Mandaka pamoja na wafanyabiashara/wachuuzi wa Soko la Mwanga.
DCEA Kanda ya Kaskazini iliwahamasisha wananchi wa Wilaya ya Mwanga washirikiane na Mamlaka katika mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za wahalifu wa dawa za kulevya waliopo katika maeneo yao wanayoishi kwa kupiga bure namba ya simu 119.