Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Tamisemi, Atupele Mwambene akizungumza katika kikao cha wadau wa a elimu kilichofanyika leo NACTVET Mwenge jijini Dar es Salaam.
Meneja Programu Mwandamizi wa GPE kutoka Ubalozi wa Sweden, Stella Mayenje akifafanua baadhi ya mambo katika kikao hicho cha wadau wa elimu.
………………
Dar es Salaam.
Serikali ya Tanzania imeanza mchakato muhimu wa tathmini na maboresho katika sekta ya elimu, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha malalamiko ya muda mrefu kuhusu ubora wa elimu nchini yanapata suluhisho la kudumu.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Tamisemi, Atupele Mwambene, Serikali inalenga kuimarisha taaluma ya ualimu na kuleta mpangilio mzuri wa ajira za wanataaluma ili ziendane na mahitaji halisi ya sekta hiyo. Hatua hii ni sehemu ya jitihada za Serikali za kutimiza vigezo vya kunufaika na mradi wa Dola milioni 167 (zaidi ya Sh454.04 bilioni) kutoka Shirika la Ushirikiano wa Elimu Duniani (GPE).
Mwambene alieleza kuwa, tathmini hiyo, ambayo ilianza mwaka 2022, imehusisha mipango ya kina kuona maeneo yenye changamoto katika sekta ya elimu na kuweka vipaumbele vya pamoja ili kuwezesha mabadiliko yanayohitajika. Maeneo hayo yanajumuisha uimarishaji wa nguvu kazi ya walimu, maandalizi na usimamizi wa walimu, pamoja na kuimarisha elimu jumuishi na uwajibikaji.
Serikali imejipanga kuhakikisha inaendana na mabadiliko ya sera na mitalaa ili kufanikisha mradi huo hadi mwaka 2030. Wakati huo huo, wadau wa elimu wameweka sharti la kuongeza bajeti ya elimu hadi kufikia asilimia 20 ya bajeti ya Serikali, kama inavyotakiwa kimataifa, ili kuhakikisha mazingira bora ya ufundishaji na motisha kwa walimu.
Kwa upande wake, Meneja Programu Mwandamizi wa GPE kutoka Ubalozi wa Sweden, Stella Mayenje, amesisitiza umuhimu wa Serikali kutimiza masharti yaliyowekwa, ikiwa ni pamoja na kuajiri walimu zaidi na kuboresha takwimu za idadi ya watu, ili Tanzania iweze kunufaika kikamilifu na fedha za mradi huo.
Mpango huu wa Serikali unalenga kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya elimu na kuondoa changamoto zinazokwamisha maendeleo ya elimu nchini, huku ukilenga kutoa matokeo chanya kwa muda mrefu.