Na. Anangisye Mwateba-Morogoro
Wanajumuiya ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) wametakiwa kusambaza elimu ya uhifadhi wa misitu ya asili waliyonayo kwa watoto wadogo ambao ndio kizazi tegemewa kwa uhifadhi endelevu wa misitu.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) alipokuwa akifungua Warsha na Mkutano wa mwaka wa jumuiya hiyo Katika Ukumbi wa Edema Manispaa ya Morogoro.
Mhe. Kitandula aliongeza kuwa Tanzania inapoteza zaidi hekta ya 469,000 za misitu kwa mwaka, hivyo zinatakiwa juhudi makusudi ili kuweza kunusuru misitu yetu. Napenda kutoa wito kwa wote, kila mmoja wetu achukue nafasi yake katika kuitetea misitu yetu, ni lazima tukumbuke kuwa uhifadhi si kazi ya mtu mmoja au kikundi kimoja.
“Ni jukumu la kila mmoja wetu, kuanzia kwenye ngazi ya familia zetu hadi kwa serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali kwani kwa pamoja, tunaweza kulinda misitu yetu na kuhakikisha kuwa inabaki salama kwa vizazi vijavyo. Tunapaswa kujitahidi kutoiharibu, bali kuitunza na kuitumia kwa faida yetu na ya dunia kwa ujumla” Alisema Mhe. Kitandula
Mhe. Kitandula katika Hotuba yake alimpongeza Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi kubwa anazozifanya za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda na kuzuia uharibifu mkubwa wa hifadhi za misitu hasa ya asili kwa ajili ya kutengeneza nishati ya mkaa au kukata kuni kwa ajili ya kupikia.
Akimkaribisha Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mwenyekiti wa Bodi ya MJUMITA Bi. Rehema Ngelekele alisema kuwa Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania unakumbwa na Changamoto mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yake. Moja kati ya changamoto hizo ni wananchi wengi kutokuwa na elimu ya faida za uhifadhi wa Misitu kwa vizazi vijavyo lakini pia kuzuia mabadiliko ya tabia nchi.
Bi. Ngelekele aliongeza kuwa jamii nyingi hazina njia mbadala ya kujiongezea kipato hivyo kufanya jamii hizo kutegemea misitu kama chanzo cha mapato lakini pia kuna uwekezaji wa muda kwenye misitu ya vijiji hivyo kupelekea kufyeka miti ili shughuli kusudiwa kwenye eneo hilo ziweze kufanyika kama kilimo na ufugaji.