OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali Mhe. Mohamed Mchengerwa amemuelekeza Katibu Mkuu – TAMISEMI kupeleka Sh. Milioni 300 kwenye Kata ya Mundarara, Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kata hiyo.
Waziri Mchengerwa ameyasema hayo leo Septemba 18, 2024 wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Longido alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata ya Mundarara.
“Nimepokea maombi yenu kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda pamoja na Diwani wa Kata hii kuwa hakuna kituo cha Afya katika Kata hii na kwa namna nilivyoona idadi ya watu na muonekano wa sehemu ya Kata hii mnastahili kuwapata Kituo cha Afya.”
“Hivyo namuelekeza Katibu Mkuu TAMISEMI kulete fedha kiasi cha shilingi Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya kuanzia ya Kituo cha Afya na ujenzi wake uanze mara moja” amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Wakati huo huo, Waziri Mchengerwa amewaelekeza TARURA Mkoa wa Arusha kutoa sh. Milioni 75 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja la Mundarara lililoathiriwa na mafuriko wakati wa msimu wa mvua.
“Nimeona namna ambavyo daraja liliko kwenye korongo la Parmunya lilivyoathiriwa na mvua na hivyo fedha hizo zijenge daraja hilo vizuri ili wananchi waweze kuendelea na shughuli zao kwa amani; Pia nitaongeza shilingi Milioni 50 kutoka kwenye fungu la dharura kwa ajili ya ukarabati wa barabara ya mundarara,”amesema