Na Neema Mtuka, Rukwa
Wananchi wa mkoa wa Rukwa wametakiwa kuachana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia kama vile kuni na mkaa, ili kuepuka athari mbalimbali za kiafya na kimazingira. Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Christina Mndeme, alipokuwa akizungumza na wadau mbalimbali, wakiwemo mama na baba lishe, kuhusu kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi.
Akiwasilisha mada yake tarehe 18 Septemba 2024, Mndeme alisema kuwa kampeni hiyo imebeba kaulimbiu inayosema: *Mazingira Yetu na Tanzania Ijayo, Tuwajibike Sasa*. Lengo la kampeni ni kuhakikisha kila mwananchi anatumia nishati safi, ikiwemo gesi, ili kuokoa afya za watu na kuboresha mazingira.
Mndeme alieleza kuwa zaidi ya Watanzania 33,024 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa yanayosababishwa na uchafuzi wa hewa, kama vile pumu, vikohozi sugu, na uti wa mgongo. Aliongeza kuwa matumizi ya nishati chafu pia husababisha mimba kuharibika, na watu hupoteza muda mwingi wakitafuta kuni na mkaa.
“Ni muhimu sana wana Rukwa kuachana na kuni na mkaa ambazo zinaathiri afya zetu. Badala yake, tutumie nishati safi kama gesi ili kulinda afya zetu na mazingira,” alisema Mndeme.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake, Watoto na Makundi Maalum, Felista Mdemu, alisema wizara yake inaweka mkazo kuhakikisha wanawake wanapewa fursa za kutumia nishati safi. Alifafanua kuwa nishati safi inaboresha hali ya maisha, akisema, “Mama anapika, lakini kwa kutumia nishati safi, muda wote anakuwa msafi, na mazingira ya chakula yanabaki kuwa bora.”
Baadhi ya mama na baba lishe walioshiriki kampeni hiyo, akiwemo Rashidi Mustapha na Leah Matofali, walisisitiza umuhimu wa nishati safi lakini pia waliiomba serikali kutoa ruzuku kwenye mitungi ya gesi ili kuwasaidia kumudu gharama.
“Tunaomba serikali itupatie muda na ruzuku kwenye gesi, kwa sababu mitaji yetu ni midogo, na bado tunafanya biashara ndogo ndogo,” walisema.
Washiriki wengine waliihimiza serikali kutoa elimu ya mazingira pamoja na elimu ya matumizi ya gesi, ili kuwasaidia wananchi kuachana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji miti ovyo.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Makongoro Charles Nyerere, alihimiza washiriki wote kuwa mabalozi wa nishati safi kwa kutoa mfano mzuri kwa jamii zao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia mnamo Mei 8, 2024, ukiwa na lengo la kutoa mwongozo wa kuhakikisha nishati hiyo inapatikana kwa urahisi na gharama nafuu kwa Watanzania wote.
Mkakati huu pia unajikita katika kufikia Lengo namba 7 la Maendeleo Endelevu (SDG7), ambalo linataka kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi na endelevu kwa wote. Rais Samia ameendelea kuwa kinara barani Afrika na duniani kwa kusisitiza matumizi ya nishati safi ili kupunguza changamoto za kiafya na kimazingira.
Mndeme alihitimisha kwa kusema kuwa serikali inaendelea kufanya mazungumzo na makampuni ya gesi ili kupunguza gharama na kuhakikisha kila mwananchi anaweza kumudu kununua gesi kwa matumizi ya nyumbani.