Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Ruhila Seko Manispaa ya Songea waliotoa maeneo yao kwa ajili ya kazi ya uhifadhi wa chanzo cha maji Ruhila wakisubiri kukabidhiwa hundi zao na Waziri wa maji Jumaa Aweso(hayupo pichani)jana.
Mmoja wa wakazi wa mtaa wa Ruhila Seko Manispaa ya Songea Hassan Mbunda kulia, kwa niaba ya wenzake akipokea mfano wa hundi ya Sh.milioni 925 kutoka kwa Waziri wa maji Jumaa Aweso wa pili kulia zilizotolewa kama fidia na Serikali kwa wananchi waliotoa maeneo yao ili kupisha uhifadhi wa chanzo cha maji katika bonde la Ruhila kata ya Seedfarm manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,kushoto Katibu Mkuu wa wizara ya maji Mwajuma Waziri na wa pili kushoto Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt Damas Ndumbaro.
Katibu Mkuu wa wilaya ya Maji Mwajuma Waziri kushoto,akimsikiliza mkazi wa mtaa wa Ruhila Seko kata ya Matogoro Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma Ali Chimgege ambaye ni mmoja wa wakazi waliolipwa fidia kutokana na kutoa eneo lake ili kupisha kazi ya uhifadhi wa chanzo cha maji cha Ruhila.
………………..
Na Muhidin Amri, Songea
WAKAZI 175 wa mtaa wa Ruhila Seko Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma,wamelipwa Sh.milioni 925.33 kama fidia baada ya kutoa maeneo yao katika bonde la Ruhila ili kupisha shughuli za uhifadhi wa chanzo cha maji.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Songea(Souwasa) Patrick Kibasa kwa Waziri wa maji Juma Aweso kabla ya hafla ya kukabidhi hundi kwa wakazi hao.
Alisema,mwaka 2003 Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Songea(Souwasa), ilifanya uthamini kwa wananchi wa eneo hilo ili waache kufanya shughuli za kibinadamu katika bonde hilo kwa kuwa limekuwa linategemewa kama chanzo kikuu cha upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Manispaa ya Songea.
Kibasa alisema,wananchi 803 walifanyiwa uthamini na kuorodheshwa na malipo yao yalifanyika kwa awamu mbili ambapo mwaka 2018 Serikali ilitoa Sh.milioni 500 kwa wananchi 361 waliolipwa fidia.
Kwa mujibu wa Kibasa, mwaka 2019,Serikali ilitoa Sh.bilioni 1.41 kama fidia kwa wananchi 442 na kukamilisha idadi ya wananchi 803 ambao walikuwepo kwenye orodha ya malipo na baadaye zoezi la uwekezaji wa alama katika eneo hilo lilifanyika.
Hata hivyo Kibasa alisema,wakati wa ulipaji wa fidia ya awamu ya kwanza na pili, wananchi 207 walijitokeza na kulalamika kwamba wameachwa kwenye malipo na wengine walilalamika kupunywa.
Kibasa alieleza kuwa,kufuatia malalamiko hayo Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma iliiagiza Souwasa kushirikiana na Ofisi ya Kamishina wa Ardhi mkoa na Halmashauri ya Manispaa ya Songea kushughulikia malalamiko hayo.
Alisema,baada ya malalamiko hayo kufanyiwa kazi ilibainika wananchi wanaostahili kulipwa ni 175 kati ya 207 na kiasi cha fedha kinachohitajika ni Sh.milioni 925.33.
Katibu Mkuu wa wizara ya maji Mwajuma Waziri,amewashukuru wananchi hao kwa uvumilivu wao na kusisitiza kuwa,serikali haitegemea kupata malalamiko mengine kutoka kwa wananchi.
Amewataka wananchi wa Ruhila,kutofanya shughuli zozote za kibinadamu katika eneo hilo,bali wahakikishe wanalinda chanzo hicho kwa manufaa yao na vizazi vingine.
Kwa upande wake Waziri wa maji Juma Aweso alisema,tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan aingie madarakani miaka mitatu iliyopita amekuwa suluhu ya matatizo ya Watanzania katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Aweso,amewataka watendaji waliopewa dhamana ya kusimamia zoezi la ulipaji fidia,kuhakikisha wananchi hao wanalipwa fedha zao haraka na kutoweka mizengwe kwenye ulipaji wa fidia hizo.
“ Wananchi wamekuwa wavumilivu kwa muda mrefu na fedha hizo ni haki zao,hivyo hakuna sababu za msingi kuchelewesha malipo yao,nawaagiza kuanzia kesho wananchi wapate fedha kwenye akaunti zao”alisisitiza Waziri Aweso.
Mbunge wa Jimbo la Songea mjini Dkt Damas Ndumbaro alisema,malipo hayo ni ya tatu kufanywa na Serikali kwa wananchi wa Songea ambapo mara ya kwanza Serikali ilitoa Sh.bilioni 5.700 kwa wananchi waliopisha mradi wa EPZA.
Dkt Ndumbaro alieleza kuwa,mara ya pili ilitoa Sh. 363 kwa wananchi wa mtaa wa Pambazuko walipoisha ujenzi wa mradi wa maji katika eneo hilo,fidia nyingine ni Sh.milioni 400 zililizotolewa kupisha upanuzi wa kiwanja cha ndege cha Songea,hivyo fedha zilizotolewa kama malipo kufikia Sh.bilioni 9.600.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa mtaa huo Juma Makweta,amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizofanikisha kulipa fidia wananchi ambao walitoa maeneo yao kupisha kazi za uhifadhi wa chanzo hicho.