Na Mwandishi Wetu, Msomera – Handeni
Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) inaendelea kuwasaidia wananchi waliotoka eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kuhamia kijiji cha Msomera kwa kuwagawia chakula, ikiwa ni sehemu ya kutimiza ahadi ya kuwapa maisha bora. Wananchi hao wanapatiwa magunia mawili ya mahindi kila kaya, kila baada ya miezi mitatu, kwa kipindi cha miezi 18, ili kuwawezesha kuzoea mazingira mapya na kuanza kujiandaa na shughuli za kilimo.
Zoezi la ugawaji wa chakula linaendelea na tarehe 18 Septemba 2024, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Idara ya Maendeleo ya Jamii, Gloria Bideberi, aliongoza zoezi hilo akieleza kuwa huu ni mpango endelevu wa serikali. “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi aliyehamia Msomera anapata mahindi wakati akijiandaa na maisha mapya. Kila kaya itapata jumla ya magunia 12 kwa kipindi cha miezi 18 ya mwanzo, wakiwa wanajipanga kuandaa mashamba waliyopatiwa,” alisema Gloria.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe. Wakili Abert Msando, alisema mpango wa ugawaji wa mahindi ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa wananchi hao wanapata maisha bora zaidi, tofauti na walivyokuwa Ngorongoro ambako walikuwa wakikabiliwa na sheria za uhifadhi zinazozuia baadhi ya shughuli kama kilimo.
“Serikali imewapatia ekari 2.5 za ardhi karibu na nyumba zao kwa ajili ya kilimo, pamoja na ekari zingine tano za kulima mazao mbalimbali. Hii ni sehemu ya mkakati wa kuwasaidia kuanza kujitegemea kwa haraka,” alisema Mhe. Msando.
Moja wa wananchi waliohamia Msomera, Bw. Sabore Olemoko, ameishukuru Serikali kwa kuwapa msaada mkubwa tangu walipohamia eneo hilo. Ameeleza kuwa mbali na mashamba na nyumba, huduma za kijamii kama zahanati, shule, maji, na maeneo ya malisho zimeboreshwa. “Tunafurahia sana maisha hapa Msomera. Mahindi tunayopata yatusaidia sana wakati tunasubiri msimu wa kilimo. Serikali imefanya kazi kubwa na tuna matumaini makubwa ya kuanza maisha mapya kwa mafanikio,” alisema Bw. Sabore.
Hadi kufikia Septemba 18, 2024, jumla ya kaya 1,451 zimenufaika na mgao wa mahindi, ambapo takribani tani 945 za mahindi zimetolewa katika awamu tofauti. Serikali inaendelea kutekeleza mipango yake ya kuhakikisha wananchi wanaoendelea kuhamia Msomera wanapata msaada unaohitajika wakati wanajiandaa na msimu wa kilimo, kwa lengo la kuimarisha maisha yao na kuleta maendeleo ya kudumu.