Afisa Mtendaji wa Kata ya Kigogo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es salaam Zuhura Almasy akizungumza na mwandishi wa habari kuhusu mapambano wanayoyafanya dhidi ya uharibifu wa mazingira.
Mwenyekiti wa Mashahidi wa Maji Mkoa wa Dar es salaam Zaharani Maulid akizungumza na mwandishi wa habari akielezea mikakati yao katika mapambano dhidi ya wadau na viwanda vinavyotirisha maji mabaya.
Katibu wa Mashahidi wa Maji Dar es salaam Mzee Miraji Simba akizungumza na mwandishi wa habari akitaja hatua wanazozichukua katika mapambano ya uharibifu wa mazingira na mito.
Mwenyekiti na Katibu wa Mashahidi wa Maji Mkoa wa Dar es salaam wakionyesha uharibifu wa unaofanywa katika mto msimbazi.
………………….
NA MUSSA KHALID
Shirika la Mashahidi wa Maji Mkoa wa Dar es salaam limeisisitiza serikali kupitia Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini (NEMC) kuongeza nguvu katika kudhibiti viwanda na wadau wanaoendelea kufanya uharibifu wa mazingira hususani kwenye mito.
Akifanya mahojiano na kituo hiki leo jijini Dar es salaam Afisa Mtendaji wa Kata ya Kigogo Wilaya ya Kinondoni Mkoani Dar es salaam Zuhura Almasy amesema licha ya faini ambazo zimekuwa zikipigwa lakini sio suluhisho bado uharibifu umekuwa ukifanyika na kusababisha athari kwa wananchi.
Zuhura ameziomba Mamlaka zinazohusika na mazingira kutembelea Kata ya Kigogo ili kuweza kudhibiti adha zinazopatikana zikisababishwa na uharibifu mazingira katika mito inayozungumza kata hiyo.
‘Tunawaomba viongozi waje kuangalia eneo mambo yanayofanyika na hakuna ulazima wa hicho kiwanda kufanya kazi hapa ikiwa anachokifanya kwetu ni madhara makubwa inatokea unaona maji ya kijani jambo ambalo limekuwa ni hatari kwa afya za wananchi wa Kigogo’amesema Mtendaji Zuhura
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Mashahidi wa Maji Mkoa wa Dar es salaam Zaharani Maulid amesema kuwa lengo lao ni kuhakikisha mazingira na rasilimali maji zinakuwa salama kwani yanapotunzwa vizuri ni sehemu ya maisha ya binadamu.
Aidha amesema kama Mashahidi wa maji hawatochoka kusema ikiwemo kwa kutoa taarifa katika mamlaka husika kuhusiana na viwanda vinavyotirisha maji taka katika Mto msimbazi na Kibangu.
‘Tunaiomba serikali najua ina nguvu ya kufuatilia kukutana na wahusika ili waweze kuangalia njia mbadala ya kutirisha maji mabaya katika mito ili kuondoa changamoto kwa wananchi ya kukumbana na athari’amesema Zaharani
Naye Katibu wa Mashahidi wa Maji Dar es salaam Mzee Miraji Simba ametumia fursa hiyo kutanja hatua ambazo wamezichukua kuwa ni pamoja na kukaa na wenye Mamlaka ili kuomba kusitishwa kwa utiririshaji maji unaofanywa na viwanda katika mkoa wa Dar es salaam.
‘Mimi nilikuwa nashauri utumike mfumo wa Dawasa kwa kila kiwanda kuwe na bomba maalum linalopokea maji kutoka kwenye kiwanda Husika lakini pia kuwe na bwawa maalum ambalo maji yote yataingia kule na kutibiwa katika hatua inayofuata’amesema Mzee Simba
Hata hivyo ameiomba serikali kufanyia kazi kilio hicho cha muda mrefu ili kurejesha viumbe vya majini ambavyo vimeonekana kupotea katika maji ya mito hiyo kutokana na utiririshwaji wa maji wanayodai ya kemikali katika mito hiyo.