Mashindano ya KNK CUP 2024, yaliyoandaliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, yamefikia kilele kwa kishindo. Timu 246 kutoka Kata 17 za Wilaya ya Bukombe zilishiriki, na Chui FC kutoka Kata ya Butinzya ilitwaa ubingwa baada ya kuibuka kidedea dhidi ya Nyuki FC ya Kata ya Bugerenga. Mashindano hayo yalihitimishwa katika Uwanja wa Kilimahewa, Bukombe, tarehe 17 Septemba 2024.
Katika tukio hilo lililohudhuriwa na mamia ya wananchi, Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, alikuwa mgeni rasmi. Dkt. Biteko alitangaza kuwa mabingwa wa KNK Cup ya Bukombe na Bashungwa Karagwe Cup watakutana kwenye mechi ya kirafiki, lengo likiwa ni kuunganisha vijana na kukuza vipaj.
Bingwa wa mashindano ya KNK CUP aliibuka na zawadi ya shilingi milioni tano, huku vilabu vikubwa kama Simba na Yanga vikivuta hisia kwa kuchukua vijana wenye vipaji maalum. Mashindano haya yameonekana kama fursa muhimu kwa timu hizo kuu kuibua na kuendeleza vipaji vipya.
Waziri Bashungwa alimpongeza Dkt. Biteko kwa kujitolea kuendeleza michezo wilayani Bukombe, akisema, “Mashindano haya yamekuwa na ubora mkubwa zaidi ikilinganishwa na miaka ya nyuma. Ni kielelezo cha jinsi michezo inavyoimarisha afya na kuibua vipaji.”
Bashungwa pia alitangaza ahadi ya kutoa shilingi milioni 15 kwa ajili ya kuboresha Uwanja wa Kilimahewa, hatua ambayo inatarajiwa kuongeza mapato ya Halmashauri na kusaidia michezo zaidi. Aliongeza kuwa ujenzi wa barabara ya Ushirombo-Katoro (km 59) kwa kiwango cha lami utaanza ifikapo Disemba 2024, kuboresha miundombinu muhimu kwa maendeleo ya wilaya.
Katika hotuba yake, Dkt. Biteko alisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili kuchagua viongozi wenye uwezo wa kuwatumikia ipasavyo.
Mashindano haya yameonyesha si tu umoja, bali pia fursa kubwa ya kukuza michezo na maendeleo ya vijana nchini.