Picha kwa hisani ya Kavazi la Mtalimbo Books
………………..
Nchini Tanzania, jina la Gonche Materego linapotajwa, kati ya watu kumi, angalau nane watauliza, “Unamaanisha yule gwiji wa michezo ya jukwaani?” Ndiyo, ni yeye! Sasa ameongeza umahiri wake kwa kuithibitisha na kuiweka katika mkusanyiko wake riwaya bora ya *Bima ya Penzi*. Tukio hili liliwashuhudia wajumbe wa Kamati Maalumu ya Filamu za Kimkakati za Elimu ya Bima Tanzania, na lilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Idara ya Sanaa za Maonesho, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akipokea nakala yake, Mwalimu Gonche alisema, “Jina, picha, na maelezo yanayoitambulisha riwaya ya *Bima ya Penzi* na mtunzi wake ni mambo yaliyovuta hisia zangu. Nilijikuta nikiwa na shauku kubwa ya kuisoma, kiasi kwamba niliamua kuisaka bila kuchoka hadi hatimaye kuipata mikononi mwangu.”
Gonche Materego ni gwiji katika sanaa za maonesho nchini Tanzania, hususan kwenye michezo ya jukwaa. Ametambulika kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza na kuimarisha sanaa za uigizaji na maigizo ya jukwaani. Ana heshima kubwa kwa uwezo wake wa kuandaa, kuongoza, na kuigiza michezo inayogusa hisia za watazamaji na kuleta mijadala ya kijamii.
Kwa miaka mingi, Gonche amejiweka kwenye ramani ya sanaa nchini kama msanii mwenye upekee, akibobea katika maigizo yenye ujumbe mzito, mafundisho, na burudani.
Amejipatia umaarufu kupitia michezo mbalimbali, na ushawishi wake katika sanaa unaonekana kupitia uzalishaji wa kazi bora zinazokubalika kitaifa na kimataifa.
Gonche pia ni mwalimu wa sanaa, akiwafundisha na kuwaongoza wasanii wachanga kujifunza mbinu bora za uigizaji na kuelewa undani wa sanaa ya maonesho.
Kazi zake zimechangia kuipa thamani na heshima sanaa ya jukwaa nchini Tanzania.
Swali letu linabaki kuwa lile lile, UNAPENZIKA, UNA BIMA?