Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amewahamasisha wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma kuhifadhi mahindi ambayo hayana kiwango, zikiwemo pumba, ili kutafutiwa soko kwa ajili ya kulisha mifugo.
Amesema hayo leo tarehe 18 Septemba 2024 wakati akiwa katika ziara mkoani Ruvuma alipotembelea Kituo cha Ununuzi wa Mahindi cha Kizuka mkoani humo.
“Katika magunia 340 niliyovuna, 40 nimeacha nyumbani kulisha familia, na mia tatu nimekuja kuuza hapa Kituoni Kizuka. Takribani magunia 10 hadi 15 yamekuwa na mahindi mabovu yasiyo na ubora,” ameeleza Mkulima Bw. Bw. Nicodem Mayo.
Aidha, ameeleza wakulima wengine wameeleza kuwa huwa wanagawa bure pumba na mahindi mabovu yasiyo na ubora; au wanalisha mifugo yao kama vile nguruwe na wengine wamesema “wanatoa rushwa kwa panya mashambani” ili wasiharibu mazao yao.
Waziri Bashe amewaeleza wakulima hao kuwa Wizara ya Kilimo itatafuta masoko kwa ajili ya kuuza mahindi hayo mabovu yasiyo na ubora. “Ningewaomba muyatenge pumba magunia tofauti na mahindi mabovu magunia mengine, ili kurahisisha mahitaji ya masoko yatakapopatikana,” amesema Waziri Bashe.