Mariam Bayumi Mkurugenzi rasirimali watu Kampuni ya Said Salim Bakhresa and Co ltd na mwigizaji wa filamu Yvonne Cherrie wakizindua kampeni ya “Azam Wheat Clean Energy” ambapo mama Lishe na Baba lishe watatumia jiko lenye kutumia mafuta ya (Ethanol) wakati wakati wa kupika vyakula mbalimbali katika migahawa yao, Wanaopiga makofi ni Priyaranjan Nath Mkuu wa Masoko SSB na Victor Akim Mratibu Miradi ya Nishati na Mazingira UNIDO.
Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufian akitoa maelezo kwa viongozi mbalimbali wa SSB namna jiko hilo linavyofanya kazi.
……………….
Na John Bukuku
Kampuni ya Bakhresa Group imezindua kampeni kabambe yenye lengo la kusaidia juhudi za serikali za kupunguza utegemezi wa matumizi ya mkaa na kuni nchini. Kampeni hii, iitwayo *Azam Wheat Clean Energy*, inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuwasaidia wajasiriamali wa ngazi ya chini, hususan Mama na Babalishe.
Kampeni hiyo itaanza rasmi wiki ijayo, ambapo kwa awamu ya kwanza, wajasiriamali wapatao 500 wa Dar es Salaam watafaidika kwa kupatiwa majiko maalum yanayotumia ethanol. Kampuni inatarajia kuifikia zaidi ya Mama na Babalishe 10,000 nchi nzima katika kipindi cha muda mfupi.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufian, alisema mpango huo unalenga kuunga mkono Mkakati wa Kitaifa wa Upishi Safi kwa kipindi cha miaka 2024-2034, huku ikiendana na jitihada za kupunguza uharibifu wa mazingira.
“Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 80 ya kaya za Tanzania zinatumia mkaa na kuni kwa upishi, hali inayochochea uharibifu wa misitu. Inakadiriwa kuwa asilimia 24 ya misitu inapotea kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati isiyo endelevu,” alisema Sufian.
Bakhresa Group imeungana na kampuni ya Ethanol, ambayo inatengeneza majiko rafiki wa mazingira. Sufian aliongeza kuwa majiko hayo yatapatikana kwa bei nafuu, huku chupa ya nishati hiyo ikiuzwa kwa Sh 1,000, hatua inayokusudia kupunguza gharama kwa watumiaji wa kawaida.
Aidha, wajasiriamali watakaopokea majiko hayo pia watapatiwa taa zinazotumia umeme wa jua ili kupunguza utegemezi wa vibatari, ambavyo vina madhara kiafya na kimazingira.
Ali Asgar, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bakhresa Group, alisisitiza kuwa kampeni hiyo ni sehemu ya uwajibikaji wa kijamii wa kampuni hiyo, inayotambua umuhimu wa kusaidia wajasiriamali kubadili tabia na kuhamia kwenye nishati safi. “Tutatoa elimu nchi nzima kuhusu faida za nishati safi ili kuboresha mazingira na afya za wananchi,” alisema Asgar.
Kwa upande wake, Mratibu wa Miradi ya Nishati na Mazingira kutoka UNIDO, Victor Akim, alisema shirika lake linaunga mkono jitihada hizi na litaendelea kushirikiana na serikali katika kukuza matumizi ya nishati mbadala nchini.
Afsa Anthony, mmoja wa Mamalishe wa Buguruni, alieleza kuwa tayari ameanza kutumia majiko yanayotumia ethanol na amebaini kuwa ni rahisi zaidi kutumia kuliko mkaa, huku akifurahia mazingira safi anayofanyia kazi.
Mkurugenzi wa Uhusiano wa Bakhresa Group, Hussein Sufian akizungumza katika uzinduzi huo wa Kampeni iitwayo”Azam Wheat Clean Energy”.
Ali Asgar, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bakhresa Group, akizungumza katika uzinduzi huo.
Victor Akim Mratibu Miradi ya Nishati na Mazingira UNIDO naye alitoa maoni yake katika uzinduzi huo.