Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewataka wabunifu wa kazi za sanaa na fasihi kujirasimisha na kurasimisha kazi zao ili waweze kunufaika na mikopo inayotolewa na Mfuko wa Utamaduni na Sanaa.
Mhe. Ndumbaro ametoa rai hiyo Septemba 17, 2024 katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakati alipofungua programu ya mafunzo ya urasimishaji wa kazi za Utamaduni na Sanaa iliyoandaliwa.
Mfuko huo una lengo la kuwajengea uwezo Wasanii na Wanafasihi hao kuhusu umuhimu wa kurasimisha kazi zao, namna ya kutumia TEHAMA katika masoko, sanaa na maadili pamoja na umuhimu wa uwekaji akiba na kumbukumbu za mapato na matumizi.
“Ili upate fedha za Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ni lazima uwe umesajiliwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu Tanzania na ofisi za Hakimiliki na Hakishiriki (COSOTA), pia lazima uwe na TIN namba ya biashara na akaunti namba ya benki kwani mikopo hii kwa sasa inatolewa na Benki ya NBC na CRDB”, amesema Dkt. Ndumbaro.”
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Bi. Nyakaho Mahemba amesema mafunzo hayo ya siku mbili yatahusisha wasanii na wabunifu wapatao 100 ili kufanya mageuzi katika ubunifu kutokana na wadau hao kukosa uzoefu wa namna ya kusimamia kazi zao na kuanzisha kanzi data ya wabunifu hao ambayo itarahisisha kuwatambua na kuwapatia mikopo kwa urahisi.
Washiriki wa mafunzo hayo kwa wakati tofauti wameishukuru Wizara kupitia Mfuko huo kwa kuwapatia mafunzo ambayo yatawasaidia kunufaika na kazi zao ikiwemo kuelewa mikataba wanayoingia na wadau kabla ya kuuza kazi zao pamoja na namna ya kupata faida baada ya kurasimisha.