Awaagiza Maafisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii kutumia njia za kidijitali kutoa elimu na fursa za kiuchumi kwa wananchi.
Na WMJJWM-MAGU
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameupongeza uongozi wa Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kwa juhudi zao katika kupambana na vitendo vya ukatili hasa mimba na ndoa za utotoni Wilayani humo.
Waziri Dkt Gwajima ameyasema hayo katika Kata ya Ng’haya wilayani Magu mkoani Mwanza Septemba 17, 2024 wakati wa ziara yake ya kuhamasisha jamii kupambana na vitendo vya ukatili na kutumia fursa mbalimbali kujiletea maendeleo.
Waziri Dkt Gwajima amesema kwa mujibu wa taarifa ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, ukatili wa kimwili kwa wanawake umepungua kutoka asilimia 40 mwaka 2015 hadi asilimia 27 mwaka 2022, na ukatili wa kingono umepungua kutoka asilimia 17 mwaka 2015 hadi asilimia 12 mwaka 2022.
“Niwapongeze Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Magu kutoka kwenye takwimu za kitaifa ninyi pia inaonesha vitendo vya ukatili vimepungua kwa mfano kwa mwaka 2016 ukatili wa kijinsia umepungua kutoka asilimia 60 kwa hadi asilimia 47 mwaka 2022 huku mimba za utotoni zimepungua kutoka asilimia 28 mwaka 2016 hadi asilimia 16 kwa mwaka 2022 ” amesisitiza Waziri Dkt. Gwajima
Ametoa wito kwa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii na viongozi wa Serikali ngazi ya vitongoji, Vijiji/Mitaa, Kata na Wilaya kuendelea kuamsha ari ya jamii kushiriki katika kutoa suluhisho ya changamoto za kimaendeleo na kuzuia vitendo vya ukatili kwa kutumia njia za kidijitali kutoa elimu kwa wananchi.
Waziri Dkt. Gwajima amewataka Wataalam hao kuendelea kusimamia uanzishwaji na uendeshaji wa madawati ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo ya umma na katika masoko na kuimarisha uelewa wa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na kulinda mazingira.
Amesema katika kushirikiana na wadau hasa jamii yenyewe Serikali inaendelea kutoa elimu na kuendesha mijadala kuhusu mila na desturi kwa jamii ili kuibua mila na desturi zinazozuia ukatili ili kuziendeleza na zile zinazochochea ukatili ili zitokomezwe.
“Nitoe rai kwa viongozi, wataalam wa Maendeleo ya jamii na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kujenga mazingira rafiki ili kuwasaidia wananchi kufanya shughuli za maendeleo bila hofu wala woga wa vitendo vya ukatili.” amesema Waziri Dkt. Gwajima
Ameeleza Serikali kwa kushirikiana na wadau inatekeleza afua zinazolenga kumaliza changamoto zinazosababisha ukatili zikiwemo kuimarisha uchumi wa kaya kwa kuendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu, kutoa elimu kuhusiana na mila na desturi zenye madhara na kuimarisha mila zenye matokeo chanya, kuimarisha ulinzi wa mwanamke na mtoto katika maeneo ya umma na katika mitandao na pia kuongeza vituo vya kutolea huduma kwa wahanga wa ukatili kama vile nyumba salama na vituo vya mkono kwa mkono na kwa kiwango kikubwa kushirikisha wanaume katika kutokomeza vitendo vya ukatili.
Aidha, amesema matokeo hayo ya kupungua kwa ukatili, yanatokana na juhudi za ushirikiano zilizofanyika kati ya Serikali na Wadau wa maendeleo mbalimbali likiwepo Shirika la KIVULINI na vikundi vya kijamii vinavyopambana na ukatili kupitia Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA-I.)
Pia Waziri Dkt. Gwajima amezindua matawi ya Mashabiki wa Simba na Yanga, wanaotumia ushabiki wa mpira kuhamasisha maendeleo na kutokomeza ukeketaji, ndoa za utotoni, mimba za utotoni na ukatili wa kijinsia na amewapongeza wananchi ambao wameamua kuunganisha nguvu zao kupitia ushabiki wa mpira wa miguu na kupinga na kutokokomeza ndoa za Utotoni, mimba za utotoni, ukatili wa kijinsia na kuhamsisha maendeleo katika familia na jamii.
Naye Katibu Tawala Wilaya ya Magu Jubilate win Lawuo amesema Wilaya hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa jamii ya kupambana na vitendo vya ukatili katika maeneo yao na kutumia fursa mbalimbali zilizopo kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini Yassin Ali amesema Shirika hilo limejikita katika kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili ikiwemo ndoa za utotoni, mimba za watoto katika jamii kwa kuja na mbinu mbalimbali za kutoa elimu hiyo kwa jamii kwa kutumia makundi mbalimbali katika jamii hususani makundi ya mashabiki wa timu za Mpira wa miguu Yanga na Simba.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Ng’haya wamemshukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii na wadau kutoa elimu kwa jamii katika kupambana na vitendo vya ukatili na kutoa fursa mbalimbali za kiuchumi kwa wananchi.