Idadi ya miili ya watu walioopolewa baada ya ajali ya boti iliyozama katika Ziwa Victoria imeongezeka na kufikia watu watatu. Ajali hiyo ilitokea wakati wakazi walikuwa wakitoka katika sherehe za harusi kutoka Kijiji cha Mwiruruma kuelekea Igundu. Hadi sasa, juhudi za uokoaji na kutafuta waliopotea bado zinaendelea.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mwenyekiti wa Kijiji cha Igundu, Sumila Nyamkinda, alisema kuwa asubuhi ya leo, Septemba 17, miili miwili zaidi imeopolewa—mwanamke mmoja aliyejulikana kwa jina la Nyachungu Rasaro (39), na mwanaume aliyefahamika kama Maida Machumu (32).
“Tumefanikiwa kuopoa miili miwili leo asubuhi. Mwili wa mwanamke tuliopoa majira ya saa 12 asubuhi, na mwili wa mwanaume tuliupata majira ya saa 2 asubuhi. Miili yote imekutwa chini ya ziwa katika eneo ambapo mtumbwi ulizama,” alisema Nyamkinda.
Aidha, mwenyekiti aliongeza kuwa kila mwili unaopatikana unakabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya taratibu za maziko. Zoezi la kutafuta miili mingine mitatu bado linaendelea.