Na: Mwandishi Wetu, Dodoma.
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa siku saba kwa waombaji mikopo ya wanafunzi kufanya masahihisho ya maombi yao.
Hii inafuatilia Bodi ya Mikopo kufanya uhakiki na kubaini baadhi ya maombi yana mapungufu na hivyo kuhitaji masahihisho ili yaweze kukamilika na kufanyiwa kazi.Uwepo wa kasoro kwenye maombi hayo, umefanya maombi hayo kutokukamilika na hivyo kushindikana kuendelea kwa hatua zaidi.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, Dk. Bill Kiwia, dirisha la kufanya masahihisho litakuwa wazi kwa siku saba kuanzia Tarehe 15 hadi 21 Septemba, 2024. Dk. Kiwia amesisitiza kuwa kwa waombaji ambao watafanikiwa kufanya masahihisho, maombi yao yataendelea na hatua zinazofuata na yatafanyiwa kazi.
Pia, ametoa wito kwa waombaji wote wa mikopo kuingia kwenye akaunti zao kuona kama wamekamilisha vizuri na kwa wale watakaoona kuna haja ya kufanya marekebisho basi wayafanye haraka ndani ya siku saba zilizotolewa ili yaweze kukamilika na kufanyiwa kazi ipasavyo.