Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa akizungumza na waandishi wa habari Mkoani Arusha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha ,Paul Makonda akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha.
……………
Happy Lazaro ,Arusha .
Waziri wa nchi Ofisi ya Rais, Tawala za mikoa na serikali za Mitaa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa ametangaza kuwa jumla ya Vijiji 12, 333, mitaa 4,269 na Vitongoji 64, 274 ikiwemo vya Tarafa ya Ngorongoro ambavyo vitashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Ameyasema hayo leo mkoani Arusha,wakati akizungumza na waandishi wa habari mkoani Arusha .
Mchengerwa amesema kuwa kwenye orodha hiyo kumejumuishwa maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa tangazo la serikali ambayo pia yalihusisha Tarafa ya Ngorongoro mkoani Arusha.
“Matangazo haya yanajumuisha maeneo yaliyokuwa yamefutwa awali kwa mujibu wa Tangazo la serikali namba 673 na 674 ambayo yalihusisha pia Tarafa ya Ngorongoro.”
” Lengo la hatua hii ni kuhakikisha kuwa maeneo haya yanapata uwakilishi mzuri kiutawala pamoja na huduma za kijamii na kiuchumi zinazowiana na mahitaji ya wananchi.” amesema Waziri.
Aidha Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi huo katika kuunda serikali ya wananchi kidemokrasia ikiwa ni pamoja na kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari la mpigakura kwa mustakabali wa maendeleo na kuendeleza juhudi za serikali katika kujitafutia maendeleo endelevu.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro, Marekani Bayo amesema kuwa, anamshukuru Rais kwa kurejesha vijiji ambavyo vilikuwa vimefutwa kushiriki uchaguzi huo .
Kwa upande wake ,Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Paul Makonda amesema kuwa, atazingatia maagizo yote yaliyotolewa na Waziri ili kuhakikisha wananchi wanashiriki kikamilifu katika uchaguzi huo .