Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila
Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Veronica Mueni Nduva.
Rais wa EAAACA, Bi. Beti Kamya.
Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Bw. Crispin Francis Chalamila, ameungana na viongozi wa Kamati Tendaji kutoka Shirikisho la Mamlaka za Kuzuia na Kupambana na Rushwa Afrika Mashariki (EAAACA) kumtembelea Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Veronica Nduva.
Ziara hiyo ilifanyika Septemba 12, 2024, jijini Arusha, ikiwa na lengo la kuitambulisha EAAACA pamoja na kujadili namna ya kushirikiana katika jitihada za kuzuia na kupambana na rushwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
“Tumejadili kwa kina kuhusu ushirikiano wetu katika kupambana na rushwa, na nimeridhishwa kuona Jumuiya ya Afrika Mashariki inalichukulia suala hili kwa uzito mkubwa. Wameona kuwa rushwa ni kikwazo katika biashara na pia ni changamoto katika kufikia malengo yetu ya maendeleo. Tumekubaliana kushirikiana kwa karibu katika maeneo mbalimbali ikiwemo mafunzo, kufanya uchunguzi wa pamoja, na kubaini mali na vyanzo vilivyojificha vinavyohusishwa na matendo ya rushwa,” alisema Bw. Chalamila.
Bw. Chalamila alibainisha kuwa kufuatia makubaliano hayo, maandalizi ya kutiwa saini kwa hati ya makubaliano (MoU) kati ya wanachama wa EAC yanaendelea, na mara baada ya makubaliano hayo kusainiwa, ushirikiano huo utaanza rasmi.
“Makubaliano haya yakisainiwa, yataimarisha zaidi mapambano dhidi ya rushwa kwa kuwa tatizo la rushwa ni changamoto ya kitaifa, kikanda, na kimataifa. Kama Jumuiya ya Afrika Mashariki, tutakuwa tunapeana taarifa kuhusu vitendo vyote vya rushwa, na hii itasaidia sana katika mapambano haya,” aliongeza.
Aidha, alisema wamekubaliana kuanzisha mafunzo na uchunguzi wa pamoja ili kuhakikisha vitendo vya rushwa vinakoma kabisa, akisema kuwa ushirikiano huo utaleta usalama zaidi kwa kuwa wanaohusika na mapambano dhidi ya rushwa ni watu kutoka jumuiya hiyo.
Kwa upande wake, Rais wa EAAACA, Bi. Beti Kamya, aliipongeza Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kujadili mbinu za kutokomeza rushwa kwa upande wa jumuiya, na kukubaliana kuanzisha mkakati maalumu ambao utaleta mabadiliko chanya katika EAC.