Dar es Salaam – Serikali, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, imetakiwa kutengeneza sera rafiki zitakazoisaidia Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kupiga hatua kubwa na kuleta tija kwa Taifa katika utendaji wake.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, mstaafu Ludovic Utouh, ameeleza kuwa ni muhimu serikali kuipa ATCL uhuru wa kujiendesha kibiashara bila vikwazo vya sasa, kama vile kukodisha ndege kwa Wakala wa Ndege za Serikali. Utaratibu huu, amesema, unakwamisha uwezo wa ATCL kufanya maamuzi ya kibiashara kwa uhuru zaidi.
Akizungumza leo, Septemba 13, 2024, wakati wa akizindua kitabu cha “ATCL Business Model: A Tale of Sweet and Sour” katika Hoteli ya Peacock, jijini Dar es Salaam, Utouh amesema kwamba nchi inapaswa kuwa na sera zinazoiwezesha ATCL kujiendesha kwa uhuru kama mashirika mengine ya anga yanavyofanya, badala ya kuwekewa vikwazo vinavyobana utendaji wake.
Akitolea mfano, Utouh ameeleza kuwa nchi za Ethiopia na Kenya zimepiga hatua kubwa kwenye sekta ya usafiri wa anga baada ya kufanya mabadiliko ya sera zao, hatua ambayo imewezesha mashirika yao kujiendesha kwa uhuru zaidi na kufanya biashara yenye mafanikio makubwa.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa Serikali kuongeza idadi ya ndege ndogo ndani ya ATCL ili kupanua huduma za usafiri wa ndani ya nchi. Hii pia itawezesha shirika hilo kujiongezea faida kwa kufikia wateja wengi zaidi, hususan Watanzania wenye kipato cha kati ambao wanaweza kumudu gharama za safari za ndege. Alisisitiza kuwa kuongeza uwezo wa Watanzania hao kifedha kutasaidia sana kupanua mtandao wa ATCL na kuimarisha faida ya shirika.
Naye Jesse Kwayu ameunga mkono hoja hiyo kwa kusema kuwa ili kuongeza idadi ya Watanzania wanaotumia usafiri wa anga, ni muhimu kuhakikisha kuwa watu wenye kipato cha kati wanapewa nyongeza ya mishahara. Hatua hiyo itawawezesha kumudu gharama za usafiri wa anga na kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma hizo.
“Watanzania wengi wako kwenye kipato cha kati, na siri ya mafanikio ni kuimarisha mishahara yao ili waweze kumudu gharama za usafiri wa anga,” alisema Kwayu.