NA FAUZIA MUSSA
Ofisa kutoka Idara ya fedha za nje, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango, Mwadini Haji Kheri, amesema Serikali zote mbili zitaendelea kutafuta wafadhili wa ndani na nje ya nchi ili kuwasaidia wakulima kuimarisha kilimo chao.
Ameyasema hayo mara baada ya kukamilika kwa ziara ya kuwatembelea wakulima wa mbogamboga, matunda na viungo walio chini ya mradi wa viungo iliyolenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo, pamoja na kuangalia mafanaikio na changamoto za wakulima hao.
Alisema hatua hiyo itawasidia wakulima waliokosa fursa kupitia mradi wa viungo, na kuwaendeleza walionufaika na mradi huo.
Alisema tathmini ya ziara hiyo ilionesha kuwa fedha zilizotolewa kuendeshea mradi huo kwa mwaka 2023-2024 zilitumika ipasavyo na kuufanya mradi kufanikiwa kwa zaidi ya asilimia 80.
Mbali na mafanikio hayo mwadini alisema bado wakulima hao wanakabiliwa na chanagmoto mbalimbali zinazopelekea kukatisha tamaa ya kuendelea na kilimo ikiwa ni pamoja na bidhaa za mbogamboga kukosa bei inayokidhi gharama za uzalishaji na kuwapatia faida hasa kipindi cha msimu.
Hivyo, aliwashauri wadau wa maendeleo kuanzisha viwanda vya kusindika mazao hayo pamoja na kuiomba Serikali kuweka bei elekezi ya bidhaa hiyo ili kumnfuaisha mkulima.
“Kwakweli wakulima hawa wanatumia nguvu na fedha nyingi katika uzalishaji lakini bado masoko yanawaangusha, hali hii inawafanya kuamua kuacha mazao yaharibike shambani” alisema
Aidha aliwataka wakulima hao kutovunjika moyo na kuendelea kuzalisha wakati serikali ikiendelea kuzitafutia ufumbuzi changamoto hizo .
“Malengo ya serikali ni kuwawezesha wakulima kuhudumia soko la ndani na kuzifanya bidhaa zao kukidhi vigezo vya masoko ya nje ya nchi, hili likikamilika litaleta manufaa kwa wakulima wetu wadogowadogo.” Alisema
Sambamba na hayo Ofisa huyo aliwataka wakulima hao kufuatilia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali ili kuendeleza kilimo.
Meneja Mkuu wa Mradi wa Viungo, Simon Makobe, alisema mradi huo ulilenga kuwainua wakulima wadogowadogo kutokana na kilimo cha matunda, mbogamboga na viungo (spice), ambapo ulifanikiwa kuwafikia wakulima zaidi ya elfu 12 wakiwemo wanawake na vijana.
Alisema kuja kwa mradi wa viungo kumekuwa chachu ya wanawake na vijana kujihusisha na kilimo kwani asilimia 60 za wanufauika wanatoka katika kundi hilo.
“Mradi huu umekuwa sehemu ya ajira kwa vijana ambao kama wangebaki mtaani ingekua kichocheo cha matukio mengine ya kuhalifu, kila mkulima mmoja ameajiri vijana kuanzia wawili na kuendelea, na akina mama wengi wamehamasika kujiunga na vikundi vya kuyaongezea thamani mazao hasa katika mazao ya viungo.” Alisema Makobe
Alisema kupitia mradi huo wa miaka minee wakulima walipatiwa mafunzo mbalimbali ikiwemo kufahamu mnyororo wa thamani wa mazao kutoka kwa mkulima, muuzaji wa pembejeo, mfanyabiashara hadi kwa mlaji, pamoja na namna ya kuyachakata na kupata bidhaa nyengine zinazotokana na mazao hayo, jambo ambalo alilitaja kuongezea tija.
Alifahamisha kuwa awali wakulima hao walikabiliwa na changamoto ya maji na umeme, ambapo mradi uliwapatia sola ili kupunguza gharama za uzalishaji.
Alisema kutokana na kuwa sheria ya mamalaka ya maji (ZAWA) hairuhusu maji hayo kutumika katika kilimo, mradi uliwapatia matangi ya maji (TANK) na mfumo mzima wa maji, na kusema kuwa ni wakati wa serikali kuangalia eneo hilo kuweza kutatua changamoto hiyo ili kumpunguzia mkulima gharama za uzalishaji na kuweza kunufaika.
Hata hivyo aliwashauri wakala wa uwezeshaji wananchi kiuchumi kuwawezesha wakulima katika kuchakata bidhaa zao pale zinapozalishwa kwa wingi na kuishauri serikali kusimamia sehemu za kuhifadhia bidhaa hizo (coldroom) ili kuyafanya mazao hayo kukaa kwa muda mrefu.
Alifahamisha kuwa wakati mradi huo ukimalizika, umezalisha wakulima wa mfano ambao kwa sasa wana mashamba darasa ya kuwaendeleza wakulima wenzao.
Kutokana na mradi huo kumalizika wakulima waliotembelewa waliiomba Serikali kuwaendeleza pale walipoachwa na mradi wa viungo kwa kuwajengea uwezo wa kupambania mikopo ili kuendeleza kilimo chao.
Aidha waliomba kutafutiwa mbinu bora za kuhifadhia mazao yao hasa mbogamboga ili kuuza kwa bei nzui pale msimu unapoisha.
“tunalazimika kuuza bei ya chini, kutokana na bidhaa hiyo kushindwa kukaa kwa muda mrefu.”
Mbali na hayo waliomba serikali kutoa elimu kwa wafugaji ili kupata usalama wa mazao yao.
Katika ziara hiyo ya kuangalia tathmini ya utekelezaji wa Mradi wa viungo (Agriconect) unaotekelezwa na shirika la PDF kwa kushirikiana na CFP na TAMWA Zanzibar, wajumbe wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango waliwatembelea wanufaika wa mradi huo maeneo mbalimbali ya mikoa ya Unguja ikiwemo Kizimbani, Mahonda, Bungi,pamoja na Ukongoroni.