Na WAF – Dodoma.
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Abbott Fund Tanzania imeanzisha kituo cha mafunzo kwa vitendo cha huduma za dharura katika hospitali ya Benjamin Mkapa chenye lengo la kuokoa maisha na kupunguza athari za ajali na dharura za kiafya.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama leo Septemba 13, 2024 jijini dodoma wakati wa uzinduzi wa Miradi na Matukio mbalimbali kwenye hospital hiyo.
Amesema ujenzi na ukarabati wa kituo hicho utaongeza ufanisi wa uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kwenye ujenzi wa miundo mbinu ya huduma za afya zikiwemo dharura.
“Hii inawezekana kutokana na Serikali na wadau wa maendeleo kufanya uwekezaji mkubwa wa vifaa vya kisasa, ununuzi wa magari ya wagonjwa na kuajiri wataalam wa afya wenye ujuzi.” Mhe. Mhagama
Mhe. Mhagama amefafanua kuwa kituo hicho kimejengwa maalum kwa ajili yakutoa mafunzo kwa vitendo kwa watoa huduma za dharura, wakiwemo Madaktari, Wauguzi, na wale wa Huduma za magari ya wagonjwa (paramedics).
Ameongeza kuwa nchi inapo jiandaa na michezo ya AFCON 2027 inatahitaji sana uwepo wa wahudumu wa afya za dharura hivyo hii ni fursa itakayowezesha kupata ajira kwenye michuano hiyo.
Waziri Mhagama ameupongeza uongozi wa hospitali ya Benjamini Mkapa kwa kutumia vizuri mapato ya ndani na kuongeza vyumba vya upasuaji vitakavyo ongeza nafasi ya huduma za upasuaji na kupunguza maumivu ya kusubiri kwa wateja.
“Ni fursa kwa madaktari ambao wanasifa ya kufanya upasuaji watapata nafasi ya kufanya upasuaji kwa madaktari wote bingwa 48 ambao nieelezwa kuwa wapo hapa Benjamini Mkapa” Amesema Mhe. Mhagama.
Mbali ya pongezi kwa Hospitali pia amewashukuru wadau kutoka India waliokuja kusaidia kutoa huduma ya viungo bandia kwa watanzania bure kwa wagonjwa 300.