Na. Zillipa Joseph, Katavi
Mkoa wa Katavi ni moja ya mikoa iliyokumbwa na mlipuko wa ugonjwa wa surua kuanzia mwezi Disemba mwaka 2022 hadi Machi 2023 na kuathiri watoto hasa wenye umri wa chini ya miaka nane ambapo jumla ya watoto 343 waliugua ugonjwa huo na watoto 13 walipoteza maisha.
Mlipuko wa ugonjwa huo uliibuka kufuatia watoto kutokupata chanjo ya surua kwa zaidi ya miaka mitatu mfululizo kutokana na kuwepo kwa ugonjwa wa Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO 19).
Aliyekuwa Waziri wa Afya wakati huo mheshimiwa Ummy Mwalimu alifika katika halmashauri ya Mpimbwe Februari 23, 2023 na kukiri kudorora wa utoaji wa chanjo mbali mbali za watoto na kuwataka wananchi kuhakikisha watoto wao wanapata chanjo ya ugonjwa wa surua.
Alisema serikali ilijikita katika utoaji wa chanjo ya UVIKO 19 ili kulinusuru Taifa na ugonjwa huo.
“Katika kipindi cha miaka mitatu tumesuasua katika kutoa chanjo dhidi ya ugonjwa wa surua katika nchi hii, na tumebaini kwamba kuna watoto zaidi ya 400,000 nchini Tanzania hawajapata kabisa chanjo ya dozi ya surua,” alisema Ummy.
Mlipuko huo wa ugonjwa wa surua ulibainika katika halmashauri 19 za Tanzania Bara ambazo ni Mpimbwe, Nsimbo, Tanganyika, Mpanda, Chunya, Bagamoyo, Kisarawe, Sikonge, Nzega, Tabora Manispaa, Kalambo, Sumbawanga vijijini, Sumbawanga Manispaa, Malinyi, Ulanga, Muleba, Korogwe, Mtwara Manispaa na Uvinza ambapo kati ya halmashauri hizo iliyoathirika zaidi ni halmashauri ya Mpimbwe iliyopo wilaya Mlele mkoani Katavi.
Kufuatia hali hiyo serikali ilianza kutoa chanjo ya surua kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano na zaidi ya watoto laki nne walipata chanjo hiyo mkoani Katavi.
Mlipuko wa ugonjwa huo mwanzoni ulileta tafrani kwa wazazi na walezi ambao kwa kiasi kikubwa waliamini dawa za asili.
“Hali ilikuwa inatisha kila nyumba yenye watoto walikuwa wanaumwa. Siku moja watoto wanne walikufa katika mtaa mmoja wanaume wakasusa kuzika ikabidi wanawake tuchimbe makaburi” alisema Mariam Mteleka ambaye ni mwenyekiti wa mtaa wa Kigangoni katika kata ya Maji Moto halmashauri ya Mpimbwe.
Khalifa Abdala ni mmoja wa watu waliopoteza watoto katika mlipuko huo wa surua. Anaeleza kuwa alikuwa na watoto wanne na wote waliugua ugonjwa huo. Mtoto mdogo aliyekuwa na umri wa miezi saba alipoteza maisha.
“Niliwapeleka kupata tiba kwa mganga wa tiba asili lakini huyo mdogo hali yake ilikuwa mbaya na tukampoteza” alisema Khalifa.
Hata hivyo mkuu wa wilaya ya Mlele Alhaj Majid Mwanga alikaa na waganga wa tiba asili na kuwapa elimu sahihi juu ya ugonjwa wa surua na kuwashauri kuwaruhusu wagonjwa wanaopelekwa kwao kwa matibabu ya asili ambao kundi kubwa walikuwa ni watoto wakatibiwe hospitali.
Mratibu wa chanjo mkoa wa Katavi Stephan Kahindi amesema jamii ilielimishwa kupitia hamasa mbalimbali juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto na hali ilibadilika.
Mwaka 2024 katika chanjo ya surua na rubella iliyofanyika mwezi wa pili mkoa ulitarajia kuchanja jumla ya watoto 171,965 wa umri wa kuanzia miezi tisa hadi miaka mitano na walichanja jumla ya watoto 196,957 sawa na asilimia 115.
Mratibu huyo wa chanjo mkoa alitaja dalili kuu za ugonjwa wa surua kuwa ni vipele na homa.
Mganga Mkuu wa mkoa wa Katavi Dk. Jonathan Budenu amesema kwa mwaka huu wamepokea visa 31 tu vya ugonjwa wa surua.
Watoto 11 kutoka halmashauri ya Mpimbwe, Tanganyika 7, Mpanda watoto 8, Nsimbo watoto 2 na Mlele watoto 3.
Aidha vipaumbele vilivyotolewa na serikali kupitia Wizara ya Afya kwa mwaka 2023/2024 ni pamoja na kuimarisha huduma za kinga dhidi ya magonjwa ikiwemo huduma ya chanjo, huduma ya lishe, huduma za usafi na afya mazingira na huduma za afya ngazi ya jamii.
Kwa mujibu wa sera ya afya ya mwaka 2007 iliyotolewa na wizara ya afya na ustawi wa jamii; kifungu namba 5.3 kifungu kidogo namba (c)(i) kinachohusu kinga, serikali imetamka kuwa kwa kushirikiana na jamii na wadau wengine itaimarisha huduma za kinga zilizo na ubora, zinazojitosheleza na kutolewa kwa usawa na uwiano.
Askofu Ephraim Ntikabuze ni Mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali ya LARDEO inayotekeleza mradi wa Mtoto Kwanza katika mkoa wa Katavi, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanakamilisha chanjo zote.
Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi, na Maendeleo ya awali ya mtoto imeeleza kwamba mwelekeo wa chanjo za msingi kwa watoto wenye umri wa miezi 12-23 unaonyesha ongezeko kutoka asilimia 71 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 75 mwaka 2015/2016.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi Albert Msovela ameitaka idara ya afya kuendelea kutoa matangazo ya mara kwa mara ili kudhibiti kabisa mlipuko wa ugonjwa wa surua.