………
Happy Lazaro,Arusha .
Katika maadhimisho ya wiki ya AZAKI inayoendelea mkoani Arusha ,Shirika la Save the Children limetoa elimu kuhusu afya na lishe bora kwa wananchi katika soko la Tengeru lililopo mkoani Arusha .
Akizungumza na wananchi hao katika eneo hilo ,Meneja wa miradi Shirika la Save the Children mkoani Dodoma , Mariam Mwita amesema kuwa shirika hilo katika kuadhimisha wiki hiyo wametoa elimu hiyo ili wananchi hao waweze kupata uelewa wa kutosha juu ya kilimo bora na hai ambacho hakitumii kemikali kwa ajili ya afya zao.
Amesema kuwa, shirika hilo limefikia hatua ya kwenda sokoni kwa lengo la kusikiliza sauti za wananchi pamoja na wafanyabiashara na kuweza kupatiwa elimu juu ya kilimo hai na kuondokana na kilimo cha kutumia madawa ambayo mwisho wa siku huwaathiri watoto .
Mwita amesema kuwa,mbali na kuwapa elimu hiyo wamekuwa wakitoa elimu namna bora ya kuweza kukopesheka na kuweza kukuza uchumi wao.
“Najua kila mmoja anapambana kwa ajili ya kupata riziki ya kusaidia familia ila kikubwa zaidi mhakikishe kile mnachotafuta kiguse mtoto kwa gharama yoyote kipato kinachopatikana ni muhimu sana kiboreshe lishe ya watoto na sio kufanyia starehe tu.”amesema Mwita.
Mwita amesema kuwa, ni wajibu wao kuhakikisha wanalima kilimo hai ambacho hakitumii kemikali ili kuwawezesha kupata lishe Bora kwa ajili ya watoto wao.
“Tumekuwa tukihakikisha watoto wanapata haki zao za msingi na wanalindwa katika haki zao zote na kuhakikisha ndoto zao hazikatishwi kwa kupata ulinzi wa kutosha. “amesema.
Kwa upande wake,Afisa maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Arumeru,Martha Mzava amesema kuwa,wamekuwa wakishirikiana kwa karibu sana na shirika hilo kwa kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi na wadau kuhusu maswala ya kilimo na uwezeshaji wananchi kiuchumi.
Amesema kuwa, kutolewa kwa elimu hiyo juu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi utasaidia sana kwani endapo uchumi ukiimarika watoto watapata mahitaji yao yote sambamba na kuepukana na vitendo vya ukatili wa kijinsia .
Aidha amewataka wazazi kuhakikisha wanawalinda watoto wao pindi wanapokuwa masokoni huku akizitaka asasi za kiraia kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara juu ya ukatili wa kijinsia ili jamii iendelee kuchukua tahadhari zaidi.