Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amesema ili kuwa na tija katika kilimo, huduma za Ugani ni muhimu, zikichangiwa na utafiti na uzalishaji wa mbegu bora. Ameeleza kuwa huduma hizo ni pamoja na elimu ya kilimo cha kisasa ikiwa ni pamoja na matumizi bora ya ardhi ili kuendana na kilimo cha Mazao na mbegu husika.
“Tumeleta pikipiki na vishikwambi kwa Afisa Kilimo ili muda wote awe kazini kusaidia wakulima kuandaa mashamba, kusajili taarifa zao ili mahitaji yao yaendane na huduma zinazotolewa na Serikali,” amesema Waziri Bashe.
Ameeleza kuwa Serikali imeamua kuwekeza kwa miradi ya maendeleo zikiwemo huduma kwa wakulima, hivyo ameomba viongozi wa Mikoa na Wilaya kuendelea kutoa ushirikiano katika kufikia azma hiyo. Waziri Bashe pia amesema kuwa Maafisa Kilimo waishi katika vijiji na maeneo wanayotoa huduma ili kufikiwa kwa urahisi.
Awali, Mhe. Waziri Bashe ambaye yupo katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga alitembelea mradi wa umwagiliaji wa Nyida ambapo mabwawa 3 yanajengwa kwa gharama zaidi ya Shilingi Bilioni 55. Ameeleza kuwa ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo ambao unatarajiwa kukamilika Machi 2025.
“Namuelekeza Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Bw. Raymond Mndolwa, kuhakikisha mradi huo unaongezewa ujenzi wa ghala la kuhifadhi mavuno ya mpunga, kuweka mashine ya kukoboa mpunga huo na nyumba ya afisa wa kilimo ambayo tayari imeshajengwa. Aidha, ameelekeza pia barabara ya kilometa 7.5 kutoka barabara kuu kuelekea kwenye mradi huo ijengwe ili huduma za usafirishaji wa Mazao na ghala litakalojengwa zifikiwe kwa wepesi.