Na Mwandishi Wetu, Igunga
Waziri wa Kilimo, Mhe. Husein Bashe (Mb), amemtolea wito Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, kuwa asiwachanganye wananchi na serikali kuhusu sekta ya kilimo, akimtaka ajishughulishe na sekta nyingine. Waziri Bashe alionya kuwa hatakubali uvumi usio na msingi kuhusu sekta hiyo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kikazi wilayani Igunga, Tabora, Waziri Bashe alionyesha kukerwa na madai ya uongo ya Mbunge Mpina, akisisitiza kwamba serikali inafanya juhudi kubwa kuboresha kilimo, hususan chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
“Mimi siwezi kunyamaza wakati sekta nyeti kama kilimo inashambuliwa na watu wenye malengo ya kisiasa. Serikali haijawahi kuleta mbegu feki au wanunuzi wa mazao wanaowadhulumu wakulima. Nakuja Kisesa, wakulima watanijibu juu ya madai haya, kwani sitavumilia siasa za uongo zinazoathiri sekta hii muhimu,” alisema Waziri Bashe.
Aidha, Waziri Bashe alisema yuko tayari kukutana na wakulima wa Kisesa ili kujadili changamoto zao moja kwa moja. “Nitakwenda kuzungumza na wakulima kujua ukweli, kama kuna ukweli katika tuhuma hizi, tutajipanga upya, lakini kama ni porojo, hatuwezi kuruhusu sekta yetu muhimu ichezewe,” aliongeza.
Katika ziara yake, Bashe pia alizindua Mpango wa Kitaifa wa Kuongeza Tija katika Uzalishaji wa Pamba kijijini Mbutu, Igunga, huku akisisitiza dhamira ya serikali ya kuimarisha kilimo cha pamba kwa kuongeza miundombinu ya umwagiliaji na kugawa zana bora za kilimo.
Alisema, “Serikali imejipanga kutoa mbegu bora na dawa bure kwa wakulima kama alivyoagiza Rais Dk. Samia. Tunafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wakulima wanapata suluhisho la kudumu kwenye changamoto zao.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba, Bw. Marco Charles Mtunga, alieleza kuwa Wilaya ya Igunga inazalisha wastani wa tani 22,000 hadi 26,000 za pamba kwa msimu, huku matarajio yakiwa kufikia tani 100,000 kupitia mpango huo mpya wa kuongeza tija.
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Cornel Magembe, na Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. Sauda Mtondoke, ambao walimpongeza Rais Dk. Samia kwa jitihada zake katika kuinua kilimo na uchumi wa wakulima.
Waziri Bashe alihitimisha kwa kusema kuwa, serikali itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na kuhakikisha kilimo kinaimarika kwa kutoa elimu ya kisasa kwa wakulima, huku akiwasihi viongozi wa wilaya na mikoa kuzingatia utekelezaji wa mipango ya kilimo kwa manufaa ya wananchi.