Na. Zillipa Joseph, Katavi
Ongezeko la vyumba vya madarasa katika shule ya msingi Nsemulwa iliyopo katika manispaa ya Mpanda mkoani Katavi limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza msongamano wa wanafunzi madarasani.
Mwaka 2020 shule hiyo ilikuwa na jumla ya wanafunzi 3,370 na vyumba kumi tu vya madarasa. Hali hiyo iliathiri mtiririko mzima wa ufundishaji na ujifunzaji.
Aidha, licha la ongezeko la vyumba vya madarasa pia mgawanyo wa wanafunzi uliofanyika baada ya kuongezeka shule nyingine mbili katika kata ya Nsemulwa umechangia kupunguza msongamano huo wa wanafunzi.
Baadhi ya wanafunzi hasa waliokuwa wakichelewa shule walikuwa wakilazimika kufuatilia masomo wakiwa wamesimama kwenye madirisha nje ya darasa, hali ambayo ilikuwa ikisababisha utoro mkubwa kwani walikuwa wakishindwa kuvumilia kukaa nje kwa siku nzima na hatimaye waliishia kutoroka shule.
Hali hiyo ilikuwa ikitokea kutokana na wanafunzi waliokuwa ndani ya darasa kujaa mpaka kufika ubaoni mahali ambapo mwalimu alikuwa akisimama kufundisha.
Kufuatia vyombo vya habari kufuatilia na kutoa habari hiyo wadau mbalimbali walianza kujitokeza na kuchangia ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa.
Taasisi ya fursa ya elimu kwa wote Equip T walijenga vyumba vitatu vya madarasa na ofisi moja ya walimu.
Aidha mwaka 2022 kupitia mfuko wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) vyumba vingine vitano vya madarasa vilijengwa na ofisi moja ya walimu.
Hali hiyo ilifanya shule ya msingi Nsemulwa kuwa na jumla ya vyumba vya madarasa 16.
Ikumbukwe kuwa mwaka 2021 serikali ilianzisha kituo shikizi katika mtaa wa Tulieni ndani ya kata hiyo ya Nsemulwa kilichokuwa na vyumba vitatu vya madarasa ambayo yalitumika kwa ajili ya wanafunzi wa darasa la awali na darasa la kwanza, ambao walilazimika kutembea umbali wa kilometa nane kwenda na kurudi katika shule ya msingi Nsemulwa.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Nsemulwa Said Mbogo alisema kufikia mwaka 2023 serikali iliamua kuigawa shule hiyo na kupata shule nyingine ya Msingi Migazini na waligawana vyumba vya madarasa na ofisi za walimu na kila shule ilipata vyumba nane vya madarasa.
Aidha iliyokuwa shule shikizi ya Tulieni iliongezewa vyumba vingine sita vya madarasa na kusajiliwa rasmi ambapo sasa ina wanafunzi 602 wa kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba; tofauti na hapo mwanzo ambapo ilikuwa na wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza tu.
“Tuliwaita wazazi na kuwaambia wanaotaka watoto wao wakasome Tulieni waandikishe majina kwa hiyo tulifuata utaratibu na tukawahamisha” alisema mwalimu Mbogo.
Aliongeza kuwa shule ya Migazini nayo ilisajiliwa na walifanya mgawanyo wa wanafunzi.
Kwa sasa shule ya msingi Nsemulwa ina jumla ya wanafunzi 1,748 kati yao wavulana 847 na wasichana 901 kutoka wanafunzi 3,370.
“Naweza kusema sasa kuna unafuu katika kuwasimamia wanafunzi kwani hapo mwanzo ilikuwa unaweza ukazungumza mpaka kichwa kikauma” aliongeza mwalimu Mbogo
Alifafanua kuwa kuongezeka kwa miundombinu ya madarasa na kusajiliwa kwa shule ya msingi Tulieni (iliyokuwa shule shikizi) na kusajiliwa kwa shule mpya ya Migazini kumeleta tija kwani msongamano wa wanafunzi umepungua katika vyumba vya madarasa na utoro umepungua.
Aidha kumetoa fursa ya kuandikishwa kwa wanafunzi wapya wa darasa la awali na msingi na pia kumepunguza umbali kwa wanafunzi waliokuwa wakitoka katika mtaa wa Tulieni.
Pia imerahisisha shughuli za kiutawala katika shule zote tatu ambazo awali ilikuwa ni shule moja.
“Jambo la kufurahisha wanafunzi wote wanakuwa darasani wakati unafundisha tofauti na awali ambapo wengine walikuwa wakifuatilia masomo kwa kuchungulia dirishani” alisema.
Mratibu wa Elimu ya Msingi Manispaa ya Mpanda Victor Rutajuhumrwa amesema kwa sasa wana jumla ya shule za msingi 46 tofauti na mwaka 2021 ambapo walikuwa na shule za msingi 34.
Mkuu wa mkoa wa Katavi Bi. Mwanamvua Mrindoko amesema serikali ya awamu ya tano imeboresha miundombinu ya madarasa kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2023 ambapo mkoa wa Katavi ulipokea jumla ya shilingi bilioni 19.4 kwa sekta ya elimu.
“Kwa upande wa shule za msingi fedha hizo ziliwezesha kujenga shule mpya kumi ambazo zimesaidia kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani” alisema Mrindoko.
Christina Cheyo ni mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Tulieni anasema kwa sasa anafuatilia masomo bila kuacha kwenda shule kutokana na shule kuwa karibu kuliko awali ambapo alilazimika kutoka nyumbani saa kumi na mbili ili kuwahi namba katika shule ya msingi Nsemulwa.
“Kipindi cha masika changamoto ilikuwa ni kubwa. Mwanafunzi akiondoka mvua ikinyesha daraja letu linajaa maji inabidi mzazi ukakae darajani usubiri mtoto ili umvushe maji” alisema Bakari Msemo mkazi wa Msufini ambaye mtoto wake kwa sasa anasoma Tulieni.
Katika sura ya kwanza ya kwanza ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023, sera hiyo imetamka kwamba serikali ina jukumu la kuandaa na kuzalisha rasilimali watu kwa ajili ya Taifa.
Sera hiyo imeendelea kufafanua kuwa suala la miundombinu, uboreshaji wa mazingira ya kufundishia na ujifunzaji yataendelea kuboreshwa ili kupata uwiano unaostahili kwa manufaa ya kujenga taifa bora la baadae.
Aidha kupitia sera hiyo serikali iliendelea kuongeza ujenzi wa miundombinu ya shule, kusajili shule mpya na ilianza kutoa elimu bure kuanzia ngazi ya awali.
Mratibu wa mradi wa Mtoto Kwanza kutoka asasi isiyo ya kiserikali ya Lake Rukwa Development Organization (LARDEO) Philbert Chundu alisema kuwa asasi hiyo inaungana na serikali katika kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kupata elimu.
Chundu ameipongeza serikali kwa kuweka juhudi katika ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa.
“Ulikuwa ukipita katika shule mbalimbali hapa kwetu unakuta wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza wanasomea nje” alisema Chundu.
Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto kwa sasa ni ajenda ya ulimwengu ambapo huduma za MMMAM zinatambulika kuwa muhimu katika kufikia Malengo ya Maendeleo.
Huduma hizo ni pamoja na kutaka mtoto mwenye umri wa kuanzia miaka 0-8 kupata fursa ya ujifunzaji.
Hali hiyo sasa inapelekea watoto wanaopaswa kujiunga na shule hususan darasa la awali na la kwanza kupata nafasi ya kupata elimu kutokana na ongezeko la vyumba vya madarasa