Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara sasa inatarajia kuanza kufanya vikao vyake vya Baraza la Madiwani na kamati za kudumu kidigitali baada ya kugawa vishikwambi kwa Madiwani wa Kata zote za Wilaya ya Serengeti.
Vishikwambi hivyo vinatajwa kama mbadala wa matumizi ya makabrasha ambapo Madiwani wote watapata taarifa za vikao kupitia vishikwambi hivyo jambo litakalo punguza gharama na muda wa kusambaza makabrasha kwa Madiwani.
Akizungumza wakati wa ugawani wa vishikwambi hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Ndg. Ally Ligalawike amesema ni Halmashauri itaondokana na matumizi ya karatasi katika vikao vya madiwani badala yake utatumika mfumo wa kidigitali utakaoipunguzia Halmashauri gharama ya ununuzi wa shajala kwa ajili ya kudurufu kabrasha za vikao ambazo zimekuwa zikiigharimu Halmashauri fedha nyingi.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti Mhe. Ayub Makuruma ameipongeza Halmashauri kwa kutimiza mpango ambao ulikuwa wa muda mrefu na kuwataka Madiwani kutumia vishikwambi hivyo Kwa matumizi sahihi sambamba na kuhakikisha vinatunzwa vizuri.
Naye Mkuu wa kitengo cha TEHAMA Ndg. Jackson Wanyancha akitoa semina fupi ya matumizi ya vishikwambi hivyo amesema Madiwani hao wataunganishwa katika mfumo ambao utarahisisha upokeaji na utoaji wa taarifa mbalimbali za vikao pamoja na zile zinazohusu shughuli zao za kia siku katika Kata zao.