Balozi wa Tanzania nchini Comoro,Saidi Yakubu amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Usafiri Baharini (ANAM),Ndugu Mohamed Dahalani ambapo wamejadiliana maeneo kadhaa ya kufanyia kazi ili kuboresha usimamizi wa sekta ya usafirishaji kwa njia ya bahari baina ya nchi hizo mbili.
Ndugu Dahalani alimueleza Balozi Yakubu kuwa ANAM inakusudia kufanya kazi kwa karibu na mamlaka mwenza nchini Tanzania – TASAC na wadau wengine ili kuimarisha sekta hiyo kwa kuhimiza usajili kwa kampuni madhubuti za meli,uzingatiwaji wa sheria za kimataifa,uwepo wa usimamizi mzuri wa usafiri wa wanyama hai na ukaguzi na operesheni za pamoja za mara kwa mara.
Kwa upande wake,Balozi Yakubu alimueleza kuwa ujio wake umefanyika wakati muafaka ambapo kipaumbele ni kusukuma diplomasia ya uchumi na ili biashara ifanyike sekta ya usafiri ni kiungo muhimu zaidi na kumuhakikishia utayari wa ubalozi na taasisi za Tanzania katika kufanikisha ushirikiano ns ANAM ikiwemo elimu ya mara kwa mara kwa watumiaji wa meli zinazofanya safari zake baina ya nchi hizo.
Balozi Yakubu pia alitumia fursa hiyo kuipongeza ANAM kwa kusaini mkataba wa makubaliano na Taasisi ya Bahari ya Dar es salaam (DMI) hivi karibuni na kuongeza kuwa itasaidia katika kuzalisha wataalam wa sekta hiyo kwa nchi zote mbili.