Watuhumiwa wa usafirishaji wa dawa za kulevya aina skanka tani 1.8 Felista Mwanri (70) na mtoto wake Richard Mwanri (47) na watu wengine watu wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Sepemba 10, 2024 jijini Dar es Salaam kwa tuhuma za kusafirisha bangi zaIdi ya tani moja.
Washtakiwa wengine ni Athuman Mohamed maarufu kwa jila la Makame (58) mkazi wa Tanga, Juma Chappa (36) mkazi wa Kiwalani na Omary Mohamed (32) ambae ni dereva na Mkazi wa Buza, Dar es Salaam.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Eric Davis amedai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Godfrey Mhini kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kwa shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya kinyume na sheria.
Amedai kuwa washtakiwa wanatuhumiwa Agosti 28,2024 wakiwa eneo la Tairo Luguruni barabara ya Kwembe ndani ya Wilaya ya Ubungo walikutwa walisafirisha dawa za kulevya aina ya bangi kilogramu 1815.
Kuhusu hatua ya upelelezi ilipofikia, Wakili Davis alidai kuwa bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.
Kabla ya washtakiwa hao kusomewa shtaka, Hakimu Mhini aliwaeleza washtakiwa kuwa kesi yao ni ya Uhujumu Uchumi, hawatatakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
Hakimu Mhini aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 24,2024 kwa ajili ya kutajwa na kuangalia hatua ya upelelezi ilipofikia