Kamishna Jenerali Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10, 2024 Jijini Dar es Salaam
Picha za dawa za kulevya aina ya skanka.
……………
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imewakamata watu watano kwa tuhuma ya kukutwa na dawa za kulevya kilogramu 1,815 aina ya skanka katika operesheni iliyofanyika Agosti 28, 2024 hadi Septemba 2, 2024 katika Mkoa wa Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 10, 2024 Jijini Dar es Salaam, Kamishna Jenerali Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo, amewataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa Richard Henry Mwanri (47) ambaye ni Mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Makonde Wilaya ya Kinondoni, Felista Henry Mwanri (70) Mkulima na Mkazi wa Luguluni Mbezi Wilaya ya Ubungo ambaye ni mmiliki wa nyumba zilipokutwa dawa za kulevya.
Watuhumiwa wengine ni Athumani Koja Mohamed (58) Mfanyabiashara na mkazi wa Mkoa wa Tanga, Omary Chande Mohamed (32) dereva wa bajaji Mkazi wa Buza pamoja na Juma Abdallah Chapa (36) Mkazi wa Kiwalani.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa katika operesheni hiyo pia wamekamata gari aina ya Mitsubishi Pajero yenye namba za Usajili T551 CAB pamoja na bajaji yenye namba za usajil MC 844 CZV.
“Mtuhumiwa Richard Mwanri amekuwa akipokea dawa za kulevya za kutoka nchi mbalimbali na kuziingiza nchini kwa usafiri wa magari zikiwa zimefichwa kwa kuchanganywa na bidhaa nyingine kasha kusambaza kwa wauzaji” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.
Dawa ya kulevya aina ya skanka ni aina bangi ya kusindika yenye kiwango kikubwa cha kemikali yenye sumu aina ya Tetrahydrocannabinol (THC) ambayo inaweza kuharibu mfumo wa fahamu, akili na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo moyo, figo na ini. Matumizi ya skanka kwa wajawazito inaweza kusababisha madhara kwa motto aliye tumboni ikiwemo kuathiri maendeleo ya ubongo na kuzaliwa na uzito mdogo.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya dawa za kulevya duniani iliyotolewa nchini Austria Juni 26, 2024 imeonesha nchi ambazo zimehalalisha matumizi ya bangi, uzalishaji wa bidhaa za bangi zenye kiwango kikubwa cha kemikali ya THC umeongezeka, huku kukiwa na ongezeko la watu wenye mataizo ya akili.
Kamishna Jenerali Lyimo ametoa wito kwa wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na biashara haramu, huku akiwakumbusha vituo vya forodha vya mipakani hususani wanahusika na ukaguzi wa magari na bidhaa zinazoingia nchini kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao.
Ukamataji wa dawa za kulevya unaofanyika nchini ni matokeo chanya ya uwekezaji mkubwa unaoendelea kufanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi thabiti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kulinda kizazi cha sasa na kijacho kwa kuimarisha mapambano dhidi ya tatizo la dawa za kulevya.