Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha
Sept 10,2024
Jumla ya Wanafunzi 6,249 wa darasa la saba katika Halmashauri ya Kibaha wanatarajia kufanya mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi.
Kati ya wanafunzi hao wavulana 3,030 sawa na asilimia 48 na wasichana 3,219 sawa na asilimia 52 wanatarajia kuketi kufanya mtihani huo tarehe 11-12 septemba,2024 kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA).
Watahiniwa hao walianza na safari ya elimu hiyo kupambana na adui ujinga 2018 ambapo tarehe 11-12 Septemba,2024 Siku ya Jumatano na Alhamisi watafikia ukomo.
Afisa Elimu Msingi na Awali wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Theresia Kyara alisema watahiniwa wote wameandaliwa vizuri kwa kipindi cha miaka Saba ya Masomo yao na kwamba tayari mikondo 275 imeandaliwa kwa ajili ya kuwatahini.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha ,Leah Lwanji ametoa rai kwa wasimamizi wa mtihani huo kufanyakazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu kwenye mitihani linaloendeshwa kitaifa.
Halmashauri ya Mji Kibaha ina jumla ya shule 71 za msingi ambapo shule za serikali ni 42 na binafsi 29.