Na John Bukuku
Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, ametoa ufafanuzi kuhusu Mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Tanzania uliofanyika hivi karibuni nchini China. Akizungumza katika mkutano huo, Silinde alisema kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa agizo kwa wakulima nchini kuanza kulima kwa kutegemea maji badala ya mvua.
Waziri Silinde aeeleza kuwa, kauli hiyo ya Rais inahusu mkakati wa kukuza kilimo cha kisasa, ambapo wizara ya kilimo imepewa jukumu la kujenga mabwawa na kuvuna maji ili kuhakikisha kilimo cha umwagiliaji kinafanikiwa. “Hii ndiyo kauli mbiu yetu sasa, kama tulivyoelekezwa na Rais, kuhakikisha tunajenga mabwawa na kutumia maji kwa kilimo badala ya kutegemea mvua pekee,” amesema Silinde.
Akifafanua zaidi, Silinde amesema kuwa China imetenga kiasi cha dola bilioni 360 kwa Afrika katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Sehemu ya fedha hizi itaelekezwa moja kwa moja kwenye sekta ya umwagiliaji nchini Tanzania, ambapo mradi huo unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa wakulima.
Aidha, Silinde ameeleza kuwa katika kipindi hicho, serikali itahakikisha kuwa miradi yote ya umwagiliaji iliyopo itakamilishwa na miradi mipya itaanzishwa ili kuwasaidia wakulima kote nchini. “Tumejipanga kuhakikisha miradi yote ya umwagiliaji inakamilishwa, na miradi mipya inaanzishwa ili kuwasaidia wakulima wetu kufikia malengo,” aliongeza.
Silinde pia amebainisha kuwa mkutano huo umefungua milango kwa Tanzania kuuza bidhaa zake za kilimo nchini China, ambapo hapo awali hakukuwa na ruhusa hiyo. “Tumepata fursa ya kuuza bidhaa zetu za kilimo nchini China. Tayari tumesaini makubaliano ya kuuza mashudu na pilipili,” alisema.
Ameongeza kuwa, wakati wa ziara hiyo, serikali pia ilisaini mkataba na Mainland Group, kampuni inayojenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mafuta ya alizeti nchini Tanzania. Kiwanda hicho kinatarajiwa kusaidia kukidhi mahitaji makubwa ya mafuta ya alizeti nchini, na hivyo kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje.