NAIBU katibu Mkuu wa Sayansi na Teknolojia Prof.Daniel Mushi wakati akifungua mkutano wa mafunzo hayo.
…………
Happy Lazaro, Arusha
NCHI za ukanda wa Mashariki Afrika EAPP zimetakiwa kukaa chini kufikiria namna ya kuanza kutumia nishati mbadala ya umeme unaotokana na madini ya Nyuklia kuzalisha umeme wa uhakika ili kukabiliana na mabadiliko ya Tabia ya nchi.
Hayo yamesemwa leo mkoani Arusha na NAIBU katibu Mkuu wa Sayansi na Teknolojia Prof.Daniel Mushi wakati akifungua mkutano wa mafunzo kwa wataalamu wa nishati ya umeme kutoka makampuni makubwa ya umeme nchi 13 za ukanda wa Mashariki Afrika (EAPP).
Amesema Tanzania kuna madini mengi ya uranium ambayo yanaweza kutumika kuzalisha umeme na nchi kuwa na umeme wa kutosha na kuweza kuuziana na nchi nyingine ili kuchochea maendeleo ya uchumi wa Taifa.
Msimamizi wa mafunzo Kanda ya Afrika ATOMIC , Dkt Dennis Mwalongo amesema mkutano huo unalenga kuwaongezea ujuzi .
Aidha wataalamu hao kutoka nchi wanachama wa Eastern Africa Power Pool (EAPP) watajadili kwa wiki mbili namna ya upatikanaji wa nishati ya umeme kupitia vyanzo mbalimbali vya asili ikiwemo joto Ardhi na matumizi ya madini ya nyukilia.
“Wataalamu hawa wamekutana kwa ajili ya kujadili mahitaji ya umeme kwa kanda ya Mashariki katika kipindi cha miaka 50 ijayo ukizingatia kwamba matumizi ya umeme katika kanda ya Afrika Mashariki yamekuwa makubwa kwa sababu watu wanaongezeka”
Mwalongo amesema mafunzo hayo ya wataalamu wa nishati ya umeme,yameandaliwa na shirika la Kimataifa la nishati za Atomic pamoja na EAPP na watajadili pia makadirio ya mahitaji ya umeme katika kipindi cha miaka 50 ijayo kwa kutumia data za kidemographics (idadi ya watu) .
Amezitaja baadhi ya nchi wanachama Kama Ethiopia na Kenya ambazo zimepiga hatua kubwa katika vyanzo vikubwa vya nishati ya umeme na kuweza kuuza umeme kwa nchi nyingine jambo ambalo wataalamu hao watajadili na kuibuka na majibu ya jinsi gani nchi zingine wanachama zinaweza kuwa na vyanzo vya nishati.
Naye Katibu mkuu wa shirika la EAPP,James Wahogo alisema nchi wanachama wa EAPP zinauzalishaji Mkubwa wa umeme na wataangalia namna ya nchi hizo ziweze kupeana umeme kwa kuuziana.
“Tanzania imepiga hatua kubwa katika suala la uzalishaji wa nishati ya umeme kutoka vyanzo asili ikiwemo Gesi na tunaimani katika kipindi cha mbeleni itakuwa na umeme mwingi wa ziada na kuziuzia nchi za jirani”amesema Wahogo.
Wahogo amezitaja nchi hizo zinazounda umoja wa EAPP kuwa ni Burundi,Comoro, DRC Congo,Djibouti, Misri,Eritrea,Ethiopia, Kenya,Libya, Madagascar, Malawi,Rwanda,Shelisheli,Sudan Kusini ,Sudan,Tanzania, Uganda na Zambia.
Mmoja ya washiriki kutoka Tanesco idara ya Mipango, Mhandisi Mwandamizi Alex Heruka amesema mafunzo hayo ya kitaalamu yanalenga kufanya makadirio ya matumizi ya umeme kupitia vyanzo mbalimbali vya nishati.
Amesema kwa sasa Tanzania imekamilisha kuunganisha mifumo ya umeme kwa kujenga laini za umeme kutoka Tanzania kwenda Zambia na ipo katika hatua ya upembuzi akinifu katika nchi za Zambia , Uganda , DRC Congo ,Malawi ,Rwanda na Burundi ili pale panapotokea nchi hizo zinaupungufu wa umeme waweze kuziuzia.